Mafuta yanayoendesha uchumi Tanzania yamechakachuliwa

‪Nimemsikia Rais John Magufuli akisema pale Mbeya kuwa uchumi wetu bado unakua kwa 7%. Pia nimeona ‘Jeshi la Watetezi wa Mambo ya Hovyo (JWMH)’, likiongozwa na Bwana Mwigulu Nchemba, likirudia maneno hayo kama kasuku bila kujuwa kuwa Shirika la Fedha Duniani (IMF) ndiyo mamlaka pekee ya dunia ya masuala ya uchunguzi wa uchumi (economic surveillance). ‬

‪IMF wamesema wazi kabisa kuwa “kama sera za kiuchumi za Tanzania hazitatazamwa upya na kuboreshwa, kasi ya ukuaji wa uchumi itashuka zaidi na inaweza hata kufikia ukuaji hasi (negative growth)”. Kwa kimombo IMF waliandika “If the policies weighing on the economy are not revised urgently, the pace of the country’s economic growth may decline further or even lead to negative growth and potential risks to the balance of payments and debt sustainability”. ‬

 

Na Zitto Kabwe

Hali ya ukuaji wa uchumi wetu itaendelea kuwa mbaya kabla ya kuboreka kwa sababu nishati ya kukuza uchumi inakauka:‬

Mosi: Mauzo ya Nje yameshuka sana. Mfano dhahiri, kwenye korosho mwaka 2018 (Tanzania imepoteza USD milioni 500), mbaazi mwaka 2017 (Tanzania imepoteza USD milioni 250), bidhaa za viwanda 2017 na 2018 (Rais John Magufuli alipokea kijiti cha urais Tanzania ikiwa inauza bidhaa za viwanda kwenda nje za thamani ya USD 1.3 Bilioni (sawa na zaidi ya TZS 3 Trilioni), kwa sasa hivi tunauza USD milioni 700 tu (sawa na TZS 1.5 Trilioni). Urari wa malipo ya bidhaa na huduma umeongezeka mpaka kufikia nakisi ya USD milioni 680 mpaka mwezi Machi 2019. Mwaka unaoishia Machi 2016, Urari wa malipo (overall balance of payments) ulikuwa na nakisi ya USD milioni 241 tu.

Pili: Wafadhili wamezuia misaada na hivyo kuathiri utekelezaji wa Bajeti. Nchi mbalimbali zilizokuwa rafiki wa Tanzania zimezuia fedha za kigeni walizopanga kuipa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali. Hata taasisi kama Benki ya Dunia wamezuia fedha kuja Tanzania. Fedha ambazo zimezuiliwa na Benki ya Dunia ni pamoja na ambazo zinapaswa kufadhili miradi ya kuboresha Elimu ya Sekondari SEQIP (USD 400m Sawa TZS 920 Bilioni), TASAF III (USD 300m Sawa na TZS 660 Bilioni) na Mradi wa Maji Vijijini (USD 300m Sawa na TZS 660 Bilioni 660).

Fedha hizi zimezuiwa kwa sababu ya serikali kutunga sheria kandamizi ya takwimu kwa lengo la kumdhibiti Zitto Kabwe (baada ya kuchambua takwimu za taarifa ya BoT na kuonyesha kuwa uchumi wetu unasinyaa), ambayo inazuia kabisa ukusanyaji na utangazaji wa takwimu zozote nchini. Lakini madhara ya kumdhibiti Zitto Kabwe kwa nchi yamekuwa makubwa mno. Kukosa MAARIFA kunaiathiri nchi.

Sababu nyingine ‬ni ubinywaji wa demokrasia nchini, msingi wake mkuu ukiwa ni kuporwa kwa ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015. Kisha vitendo vya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge (Bunge Live), kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya Upinzani nchini (huku ya CCM ikiruhusiwa), na kuwabambikia kesi mbalimbali wanasiasa wa upinzani, kupigwa risasi kwa Mbunge Tundu A. Lissu akiwa kwenye eneo la Bunge mjini Dodoma, kuwanyima fursa ya kurudi kusoma wasichana waliopata ujauzito shuleni, na Kutungwa kwa sheria mpya ya vyama vya siasa inayoua kabisa siasa za vyama vingi nchi.

Mfululizo wa matukio hayo yanayouwa demokrasia yetu umepelekea nchi wahisani (wafadhili) kutoleta fedha za kigeni nchini. Pia uminywaji huu wa demokrasia pamoja na matukio mengine ya ukandamizwaji wa haki za binadamu vimesababisha mahusiano ya Tanzania na nchi zinazofadhili na kuchangia Bajeti na hata mashirika ya kimataifa kudorora. Baadhi ya mashirika na nchi zikifuta kabisa misaada na huku wengine wakizuia au kuchelewesha kutoa fedha za kusaidia bajeti yetu ya Maendeleo.

Tatu: Kupungua kwa uwekezaji nchini (FDI) kunapekelea shughuli za uchumi hapa nchini kutoongezeka, na hivyo kutozalisha ajira rasmi za kutosha na kutoongeza mapato ya serikali. Taarifa ya Benki ya Dunia (Economic Update No. 11) inaonyesha kuwa Tanzania Uwekezaji kwa uwiano wa Pato la Taifa (GDP) umeshuka kutoka 5% ya GDP mwaka 2015 mpaka 2% ya GDP mwaka 2018. Hii maana yake ni kuwa jumla ya shilingi Trilioni 4 zimeondoka kutoka uchumi wetu katika kipindi cha miaka mitatu tu.

‪Sababu hizo tatu, (Mauzo Nje, Wafadhili pamoja na Uwekezaji Mitaji (FDI)) ndio nishati ya kuendesha ukuaji wa uchumi. Ni kama gari na mafuta ya dizeli, unaweza kuwa na gari jipya lakini halina mafuta, halitafika popote. Pia gari hiyo ikiwa na mafuta kidogo haitakufisha mbali unakokwenda. Kasi ya ukuaji wa uchumi wetu imeporomoka kwa sababu serikali ya CCM ya Awamu ya 5 chini Rais John Pombe Magufuli inakata nishati ya kuendesha uchumi kwa kuweka sera fyongo. Mafuta yanayotumika kuendesha uchumi wetu Hivi sasa yamechakachuliwa (adulterated fuel).

‪Serikali kwa sasa inategemea mikopo kutoka mabenki ya kibiashara, na inadhani kuwa mikopo ya kutoka mabenki ya biashara ya nje itaweza kuziba pengo la nishati niliyoeleza hapo juu, HAIWEZEKANI. Kwa mfano, hivi sasa serikali imekubaliana na Benki ya Standard Chartered kupata mkopo wa USD 1.5 Bilioni (sawa na thamani ya fedha za kigeni za mauzo yote ya nje ya bidhaa za viwandani aliyoyakuta Rais Magufuli wakati anaingia madarakani) kwa ajili ya mradi wa Reli (SGR), na Benki ya Credit Suisse kupata mkopo wa USD 500 milioni (sawa na fedha zote za kigeni tulizozipoteza kwenye korosho msimu uliopita) kwa ajili ya miradi mingine ikiwemo Stiglers Gorge.

Lakini Watanzania hamuambiwi kuwa mikopo hii kutoka mabenki ya kibiashara ya kimataifa ni ghali mno kwa kuwa ina riba kubwa na ni ya muda mfupi (kwa maana miradi ambayo fedha hizo zitatumika kuifanya itakuwa haijakwisha wakati mkopo utakapoanza kulipwa). Mikopo hii ghali kamwe haiwezi kuwa mbadala wa Nishati hizo tatu tulizozichakachua.

‪Rais Magufuli akubali tu kuwa amesimamia uharibifu mkubwa wa uchumi wa nchi yetu na hivyo apishe watu wengine watakaoweza kurudisha uchumi wetu kwenye reli sahihi. Ni aibu kubwa kukabidhiwa nchi yenye uchumi unaokua kwa 7% kwa miaka 10 mfululizo halafu wewe ndani ya miaka mitatu unaupeleka uchumi huo kwenye msinyao (negative growth). Rais Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri hawapaswi kuwa Ikulu, bali wanapaswa kuwa kizimbani kujibu mashtaka ya uhujumu uchumi (economic sabotage). ‬

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii, Kabwe Z. Ruyagwa Zitto, ni kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.