Ghafla maneno ya Mdude Chadema yamenipa nguvu mpya

TAKRIBAN saa 24 zimepita nikiwa natetemeka na kunyongea kwa uoga. Nilikuwa kama kuku aliye bandani anayengoja zamu yake ya kuchinjwa. Ni baada ya kuku wenzangu kuchukuliwa kwa zamu. Alianza Alphonce Mawazo, akafuata Ben Saanane, akaja Azory Gwanda, Daniel Yona wa Kinondoni, Simoni Kanguye na wengine, lakini sasa tunaumizwa kutekwa kwa ndugu yetu Mdude Chadema.

Swali lilikuwa je, zamu yangu ni lini? Nimeteseka kwa siku nzima bila kupata majibu. Kadiri nilivyowaza ndivyo nilizidi kuwa mpole na kunyong’onyea zaidi.

Ghafla nikakumbuka Mawasilaino yetu watu watatu; Mimi, John Heche (mbunge) na Mdude Nyagali (Mdude Chadema).

Na Jacob Boniface

Miezi kadhaa iliyopita Mdude alitushirikisha mimi na Heche kuhusu SMS kadhaa alizokuwa akitumiwa na watu waliojitambulisha kuwa wanatoka kwenye vyombo vya dola. Kupitia SMS hizo, watu hao walijiapiza kummaliza.

Walimwambia sababu ya kummaliza ni kwamba mateso waliyompa awali hayakusaidia kumrusisha nyuma katika harakati zake, hivyo waliona dawa sahihi ni kumuua.

Mdude aliwahi kusafirishwa kutoka Songwe mpaka Dar usiku kucha. Alipofikishwa Dar alifungiwa kwenye nyumba moja ya siri na yenye mateso makali. Nyumba hiyo ipo Mikocheni. Pamoja na mateso yote waliyompa, Mdude hakurudi nyuma. Aliendeleza harakati.

Sasa basi, siku hiyo mimi na Heche tukimsikiliza, alitueleza kuwa jamaa waliomtumia hizo SMS walikuwa wakimsumbua sana na walisisitiza azma yao ya kumuua. Akasema, mara kadhaa alijulishwa kwamba watekaji waliingia kimyakimya mji mdogo wa Vwawa, Songwe ili kumshughulikia.

Mdude alipotushirikisha hayo, aliomba mimi na Heche tumsaidie, kwani tayari alishatoa taarifa polisi mara kadhaa lakini alikuwa hajioni kama yupo salama.

Mimi na Heche tulimshauri akimbie, siyo tu Songwe, bali ikibidi nje ya nchi kabisa akajifiche. Heche alitoa msaada wa makazi ya atakapo kimbilia Mdude. Alimuunganisha na mwanasiasa mmoja wa Kenya ambaye alikubali kumpokea na kumpa mahitaji muhimu jijini Nairobi.

Mimi nilimsaidia maarifa ya namna ya kuwatoroka hao watekaji. Vilevile namna ya kuyakwepa mawasiliano waliyokuwa wanayatumia kumfuatilia. Akapata kadi mpya ya simu. Siku iliyofuata alianza safari kwa kuunganisha magari ya mizigo na abiria mpaka afike uhamishoni, Nairobi, Kenya.

Mdude alifanikiwa kufika Arusha. Alifikia kwa kamanda ambaye ni msiri wetu. Huyo kamanda ndiye alikuwa na jukumu la kuhakikisha Mdude anavuka boda salama na kuingia Kenya.

Ghafla Mdude alinipigia simu. Aliniambia ameghairi kwenda Nairobi na kwamba kesho yake angegeuza kurudi Vwawa, Mbozi mkoani Songwe.

Nilichoka kabisa. Niliongea na Heche. Tukachoka zaidi. Juhudi zote zile za kumtorosha, amefika Arusha na kuamua kurejea Songwe. Mimi na Heche tulijaribu kumshawishi lakini alikataa katukatu.

Nilijaribu kumkumbusha hata Maumivu ya mateso ya awali aliyoyapata wakati njia yake ya Mkojo inavuja damu,maumivu makali ya kila sehemu za mifupa ya mikono na Vidole baada ya kutoka nyuma ya Mateso

Hatukumwelewa kabisa. Hata yeye alijua tumekasirishwa na uamuzi wake wa kurudi kwao Vwawa.

Leo nimeyakumbuka maneno yake aliyosema wakati anasisitiza uamuzi wake wa kughairi kwenda Kenya. Maneno hayo yamenitoa machozi. Yanenipa nguvu na tabasamu.

Mdude alitueleza mimi na Heche, namnukuu: “Nimetafakari sababu ya mimi kukimbia nchi yangu hainipi kabisa. Roho na dhamira vinanisuta kuwa nikikimbia watekaji kwa sababu ya kukosoa Serikali namwachia nani hili jukumu? Huyo atakaye fanya na yeye pia si binadamu kama mimi? Hana ndugu? Hapendi kuishi? Narudi nyumbani najua wataniua au kunipoteza, lakini acha wafanye hivyo nikiwa katika nchi yangu.”

Mdude aliendelea kusema: “Najua kaka zangu nimewakwaza kwa uamuzi wangu wa kurudi nyumbani hasa baada ya siku tatu za kuwasumbueni mnisaidie. Msihofu hao jamaa hawawezi kutuua wakatumaliza sisi sote. Hata kama kila siku watateka mtu mmoja basi itawabidi kutumia miaka mitano kuteka watu 1500 wakati sisi tupo milioni 50. Bado sisi hatupaswi kuwaogopa wao, kwani hawana uwezo wa kutumaliza wote.”

Ni maneno hayo ya Mdude yaliyonitoa machozi lakini yakanipa nguvu. Nikasema Mdude ameshinda. Mdude ndiye mshindi. Acha wamfanye lolote lile lakini kamanda ameshinda hii vita.

Kwa maana aliwajua, akajua watakachokifanya na akajiandaa vema bila ya kuogopa. Alichagua kuitetea nchi yake kwa gharama ya uhai wake.

Hata mimi natamka leo. Nipo tayari kwa lolote. Sitaikimbia nchi yangu. Sitakimbia wajibu wangu. Nitakufa kwa ajili ya nchi yangu.
Je wewe Upo tayari?

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Mstahiki Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii leo tarehe 6 Mei 2019

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.