Kuna tafauti kubwa kifo cha Mengi na cha Ruge

INAFUNDISHWA kwenye Msahafu, sura ya 67 (Ufalme) kuwa kifo na uhai ni mtihani ambao Mungu ameuweka kwa waja wake ili kupima ufaulu wao. Ufaulu unaosemwa na Mungu ni matendo, je, nani ataogopa kifo ili atende mema na kumcha Mungu?

Hiyo ni thiolojia ya uhai na kifo katika Msahafu. Ukitafsiri kifo na uhai katika falsafa ya kijamii, unapata jawabu lilelile kuwa kifo na uhai ni mtihani. Kuna wanaokufa wamefaulu, wengine wanafeli, wapo hukatishwa mitihani. Wengi hujifelisha.

Kijamii chumba cha mtihani ni uhai. Na kifo ndiyo hutoa tafsiri ya ufaulu. Wapo hupata ufaulu mkubwa. Wengine hufaulu kidogo. Wapo huondoka duniani na matokeo ya wastani. Hawakosekani wenye kufeli. Kuna watahiniwa hunyimwa fursa ya kuingia chumba cha mtihani.

Na Luqman Maloto

Mimba ambazo hutolewa ni tafsiri ya watahiniwa ambao hunyimwa fursa ya kuingia chumba cha mtihani. Uhai wao ndiyo uwepo wao kwenye chumba cha mtihani. Angalau wangeruhusiwa kuingia duniani, wangejibu maswali kadhaa ya mtihani wao.

Vifo vya watoto katika umri wowote, ni matokeo ya watahiniwa kuondolewa chumba cha mtihani kabla ya kukabidhiwa karatasi ya majibu. Vijana wadogo wanapofariki dunia, ni kielelezo cha watahiniwa ambao walikosa muda wa kutosha kujibu maswali ya mtihani wao.

Hapa sasa ifahamike kuwa kuua ni dhuluma kubwa. Maana unamkatisha mtu kujibu maswali ya mtihani wake. Unamuondoa chumba cha mtihani, wakati kumbe angefaulu vizuri. Hata wale ambao wangefeli, wanapouawa hulaumu waliowaua, kwamba wangepata muda mzuri wa kujibu maswali ya mtihani wao wangefaulu.

Marehemu Steven Kanumba

Vifo vya vijana wenye kuonesha matokeo bora ni ishara ya watahiniwa kuishiwa wino chumba cha mtihani, ingawa bado walikuwa na muda wa kutosha wa kuendelea kufanya mtihani wao. Kuna wale hunyang’anywa kalamu wasiendelee kufanya mtihani.

Steven Kanumba aliishiwa na wino kwenye chumba cha mtihani. Akatoka akiwa kijana mdogo. Dalili zilikuwa njema kwamba angepata muda wa kutosha, ufaulu wake ungekuwa mkubwa. Wastani wa alama alizokusanya akiwa kwenye chumba cha mtihani kwa uwiano wa muda alioutumia, bila shaka alipata ufaulu mzuri.

Albert Mangweha ‘Ngwair’, wino uliisha katikati ya chumba cha mtihani akiwa hajajibu maswali mengi. Kwa ambayo aliyajibu, jamii inaweza kuona ufaulu wake. Aliihudumia jamii ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa muziki mzuri.

Jiulize Tupac Shakur angepata ufaulu upi kama angepata umri wa japo miaka 40 ndani ya chumba cha mtihani? Ikiwa aliishi miaka 25 na miezi mitatu kasoro siku tatu, mpaka leo anaimbwa kwa mapinduzi aliyoyafanya kupitia harakati zake za muziki wa Hip Hop, angeongezewa miaka 25 ingekuwaje?

Kwa vile Tupac aliuawa kwa kupigwa risasi, bila shaka kilio chake ni kunyang’anywa kalamu wakati alikuwa bado na majibu ya kutosha kuhusu mtihani wake. Hii inaleta mantiki kwamba wapo watu wengi malalamiko yao yatakuwa ni kunyang’anywa kalamu wakiwa na majibu ya kutosha au kupewa kalamu ya wino mchache kuliko wengine.

Marehemu Albert Mangwair

Kuna wale hujiua. Hao ni watahiniwa ambao hujiondoa wenyewe chumba cha mtihani. Wanaona maswali magumu badala ya kujaribu kujibu, wanachagua kukimbia. Huwezi kumbebesha lawama mtu mwingine wakati umeshindwa mwenyewe mtihani. Pengine wangeruka maswali waliyoona magumu na kukimbilia mengine mepesi labda wangefaulu.

Hapa ni kuonesha pia kuwa wakati wapo ambao kalamu zao zilikuwa na wino kidogo, hivyo kuishia njiani ndani ya chumba cha mtihani, wengine kalamu zao zina wino wa kutosha lakini walikimbia mtihani. Vijana waliotwaliwa wakiwa wadogo na kushindwa kujibu mtihani ipasavyo, watawalaumu waliojiua, kwani hawakutumia ipasavyo wino wa kalamu zao.

King Majuto alikuwa msanii mkubwa Tanzania. Alipata muda mzuri wa kujibu mtihani ndani ya chumba cha mtihani. Huwezi kumlinganisha na Sharo Millionaire ambaye wino uliisha mapema na kujikuta akiondolewa chumba cha mtihani, wakati alitamani kuendelea kujibu maswali na pengine majibu alikuwa nayo ya kutosha.

Kuna ambao hufaulu mtihani mapema na huendelea kubaki chumba cha mtihani ili kuongeza alama za ufaulu na kuulinda ufaulu wao. Barack Obama, ana umri wa miaka 57. Umri ambao alikuwa nao Benjamin Mkapa alipokuwa anaapishwa kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1995. Sawa na umri wa Rais John Magufuli, alipochaguliwa kuwa Rais Oktoba 2015.

Marehemu Sharo Milionea

Katika umri wa miaka 57, tayari Obama alishaihudumia Marekani katika nafasi ya Urais. Kijamii, hata sasa Obama ameshafaulu. Hata hivyo, kwa vile kalamu yake bado ina wino, basi anaendelea kuongeza majibu kwenye mtihani wake.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alifariki dunia mwaka 1999. Alikuwa na umri wa miaka 77. Mwalimu Nyerere aliondoka chumba cha mtihani akiwa amefaulu kwa kiwango kikubwa. Aliikomboa nchi, akaikomboa Afrika, akailea Tanzania, akawalea viongozi wa Afrika. Kalamu ya Mwalimu Nyerere ilikuwa na wino mwingi, na alijibu maswali karibu yote ya mtihani wake na kufaulu vizuri.

Mengi na Ruge

Reginald Mengi aliishi duniani miaka 77, yaani kutoka mwaka 1942 mpaka 2019. umri sawa na Mwalimu Nyerere. Mengi aliitafuta elimu na kuipata. Mwanzoni baada ya kutoka Ulaya masomoni, aliajiriwa lakini akachagua kuwa mfanyabiashara. Akafanya biashara na kupata alama A. Akawa tajiri, bilionea mkubwa.

Mengi akawa mlipa kodi mkubwa nchini. Akafanya kazi nyingi za kijamii ili kuiendeleza jamii ya Tanzania. Hakuwa tu mfanyabiashara bali pia mwendeleza biashara. Hakumiliki viwanda peke yake, isipokuwa alikuwa mwendeleza viwanda. Hakuishia kumiliki vyombo vya habari, ila alisimama kama mtetezi na mwendeleza tasnia ya habari.

Ungemuona Mengi akipiga vita matumizi ya zebaki migodini ili kuokoa maisha ya watu wanaoishi kuzunguka migodi na wachimbaji wadogo. Mengi alisimama kama mtetezi wa mazingira na alikuwa alama ya mapambano dhidi ya Ukimwi. Alikuwa mkono wa walemavu na yatima. Aliwapigania albino.

Marehemu Mzee Majuto

Alipenda kuwajengea uwezo vijana kujiamini na kutumia vipaji vyao kufanikiwa kwenye maisha. Aliwapa mitaji wale waliokuwa wanaonesha kuwa na mawazo mazuri. Zaidi, Mengi ameacha ngome nyingi imara za kibiashara.

Maisha kama chumba cha mtihani, basi Mengi amejibu maswali mengi na kwa ufaulu wa hali ya juu. Uhusika wake kibiashara na kijamii kwa jumla, unadhihirisha kwamba kalamu ya Mengi ilikuwa na wino wa kutosha. Na aliitumia vizuri kujibu mtihani wake. Wino umeisha. Na amefaulu sana.

Kwa umri wa miaka 77 aliyoishi, ni jibu gani jipya Mengi angeliweka kwenye mtihani wake likawa la ajabu kupita yale aliyoyaweka? Vema kumshukuru Mungu kuwa Mengi ni kati ya binadamu wachache ambao walipewa kalamu zenye wino mwingi kujibia mtihani na walizitumia ipasavyo.

Ruge Mutahaba alikuwa mpiganaji hasa. Miaka 49 kasoro miezi miwili aliyoishi duniani, kalamu yake iliandika majibu mengi ya mtihani wake. Kuanzishwa na kukua kwa ngome ya Clouds Media Group (CMG). Hakuwa tu mdau wa sekta ya habari na burudani, bali alikuwa mwendeleza sekta.

Ruge aliwapa mwanga vijana waliokuwa gizani kuhusu vipaji vyao kupitia taasisi ya Tanzania House of Talent (THT). Mradi wa Fursa aliutumia kuwajaza ari ya ujasiriamali na kujikomboa kiuchumi watu wa rika na jinsia zote. Ruge pia alikuwa mwenye kumulika wenye shida na wakata tamaa kisha kuwapa matumaini.

Ukiyapima aliyofanya Ruge unaona kuwa kalamu yake aliitumia vizuri kuweka majibu sahihi kwenye mtihani wake. Hata hivyo, wino ulimwangusha Ruge. Alitamani angepata kalamu yenye wino zaidi ili aendelee kujibu mtihani. Jinsi Ruge alivyoaga dunia, unaona kuwa alikuwa na kiu ya kuendelea kubaki chumba cha mtihani. Wino ulimgomea.

Tofauti ya kifo cha Mengi na Ruge ni wino. Mengi alijibu maswali mengi ya mtihani wake. Ameondoka chumba cha mtihani akiwa na ufaulu mkubwa. Majibu ambayo ameondoka nayo kichwani pasipo kuyaacha kwenye karatasi ya majibu ni machache. Wino umemtendea haki Mengi.

Ukipima ufaulu kwa yale ambayo Ruge alifanya, bila shaka amefaulu vizuri, ila alihitaji wino zaidi. Ruge ameondoka na majibu mengi ya mtihani wake ambayo hakuyaweka katika karatasi ya majibu. Wino haukuwa mshkaji kwa Ruge.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.