Kangi arudishwe chuoni kusoma lugha ya uongozi

MIAKA  45 iliyopita, yaani mwaka 1964, aliyekuwa mhadhiri wa saikolojia wa Chuo Kikuu cha Cornell, New York, Marekani, Michael Beldoch, alifanya utafiti na kuweka kwenye maandishi somo linaloitwa “emotional intelligence”.

Mwaka 1995, mwandishi wa habari za sayansi nchini Marekani, Daniel Goleman, alitoa kitabu akakiita “Emotional Intelligence”. Ndani ya kitabu hicho, Goleman anaeleza kinagaubaga maana ya emotional intelligence na uwanda mpana wa ufanyaji wake wa kazi.

Emotional intelligence ni uwezo wa kisaikolojia kutambua hisia zako na kujua namna ya kuzidhibiti na vilevile kuwa na ufahamu wa namna ya kuzungumzia hisia za wengine kwa haki. Kwa kifupi emotional intelligence ni kutambua hisia zako pamoja na wanaokuzunguka.

Na Luqman Maloto

Emotional intelligence imekuwa ikiingizwa mara nyingi katika masomo ya uongozi, yaani Emotional Intelligence in Leadership. Kwamba kiongozi sharti awe na uwezo wa kudhibiti hisia zake na kuheshimu za wanaomzunguka. Kiongozi hupaswa kuonekana mtulivu na mjenga hoja zenye kuleta mantiki.

Tukienda ngazi kwa ngazi, emotional intelligence in leadership inamjenga kiongozi kuwa na lugha ya uongozi, yaani leadership language. Kiongozi haipendezi awe anatoa maneno kama mpigadebe wa kwenye vituo vya daladala.

Watu humtafsiri kiongozi kulingana na maneno anayozungumza, lakini zaidi kwa matendo yake. Kiongozi hupaswa kuwa mtulivu katika vitendo vyake, na awe anachagua maneno anapofanya uwasilishaji. Kinachotoka kinywani mwa kiongozi, hubeba tafsiri ya jinsi anavyojitambua au asivyojitambua.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipata kusema, ukipewa kazi ya wananchi lazima ujiheshimu. Kujiheshimu ni kumaanisha kuheshimu wanaokuzunguka. Huwezi kuheshimu watu kama hujiheshimu. Vilevile, kutojiheshimu ni kutoheshimu wengine.

Kauli za Kangi Lugola

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, alisema kuwa hajapata kuona mtu mwongo kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad. Kangi alisema CAG amepotosha kuhusu kashfa ya sare hewa za jeshi la polisi zenye thamani ya Shilingi bilioni 16.

Akafafanua kuwa yupo tayari kuvua nguo kama ikithibitika aliyosema CAG ni kweli. Kauli hizi: moja ya “kuvua nguo” na ya pili “hakuna mwongo kama CAG” ndizo zinatuleta kumtafakari Kangi kama anajua matumizi sahihi ya lugha ya uongozi.

Kwanza, “kuvua nguo” ni viapo vya mtaani. Wanaotaniana habari za mpira hufyatuka “Simba ikichukua ubingwa nitavua nguo sokoni Kariakoo”. Maneno ya hivyo hayawezi kusemwa katika ya kada mbili au tatu zenye kutarajia heshima isiyo na punguzo.

Baba hawezi kumwapia mwanaye kuwa “ulivyo huna akili ukifaulu hisabati nitavua nguo barabarani”, au mama amwambie binti yake “unavyoendekeza uhuni badala ya shule mwaka huu usipotuletea mimba nyumbani nitavua nguo ndani ya daladala.” Viapo vya mitaani haviwezi kutumiwa nyumbani baina ya wazazi na watoto.

Kuvua nguo si kiapo cha uongozi kwa taifa. Inasikitisha zaidi, Kangi aliyasema hayo maneno bungeni. Nyumba adhimu kabisa kwenye nchi. Hivyo, Kangi anapaswa kuelewa kuwa yapo maneno hayafai kutamkwa bungeni, muhimu zaidi maneno ya mtaani na vijiweni, yabaki hukohuko, yasibebwe na kutamkwa na viongozi.

Katika lugha ya uongozi, jumlisha na ukosoaji wa kiungwana. Inashauriwa usimparamie mtu na kumshambulia binafsi, jadili hoja au wazo alilotoa. CAG ametoa ripoti ya ukaguzi alioufanya kikatiba. Kama unaona kuna ufafanuzi wa kutoa, fanya hivyo bila kumshambulia yeye binafsi. Kangi amemwita CAG mwongo kupita waongo wote. Si kauli ya kiongozi. Mbaya zaidi ameizungumza bungeni.

Ukosefu wa uungwana

Katika ukosoaji wa kiungwana inafundishwa pia heshima wakati wa kukosoa. Unapaswa kuangalia unayemkosoa ni nani? Umri wake? Ana daraja lipi? Huwezi kumkosoa mzee kama ufanyavyo kwa kijana mwenzako. Mwanafunzi hawezi kumkosoa mwalimu wake kama afanyavyo kwa mwanafunzi mwezake. CAG Assad ni profesa, Kangi akimkuta chuo kikuu, atamfundisha, atampa mtihani, atamsahihisha na akiamua atamfelisha.

Zaidi, CAG siyo tu mkaguzi bali pia ni mdhibiti wa fedha za Serikali. Ukitambua nafasi ya CAG kikatiba huwezi kuongea maneno dhidi yake bila udhibiti. Kiongozi mwenye lugha ya uongozi, atachunga maneno anapomzungumzia CAG.

CAG anapofanya ukaguzi, hahitimishi pasipo kupata majibu ya Serikali. Majibu yanapokosekana ndipo hutaja udhaifu wa kimahesabu. Na kwenye ripoti CAG ameeleza namna ambavyo aliomba uthibitisho wa manunuzi ya sare hizo na kukosekana. Kangi anasema sare zipo kwenye makontena bandarini. Hata hivyo, polisi walishindwa kumjibu CAG ipasavyo.

Zingatia, ripoti ni hesabu za Serikali mpaka Juni 30, mwaka jana. Huu ni mwaka mwingine wa fedha na umebakiza miezi miwili uishe, Kangi anasema sare zipo kwenye makontena. Tangu hesabu za mwaka uliopita, mpaka leo bado tu kwenye makontena? CAG hakagui makontena, anakagua nyaraka. Na nyaraka alizooneshwa zilionekana kuwa na upungufu. Na alizoomba hakupewa.

Kangi ndiye aliyesema bungeni mwaka jana kuwa wabunge waache kuhoji watu wanaokufa vituo vya polisi, akahoji mbona wanaokufa nyumba za kulala wageni katikati ya mapenzi hawahoji? Kweli hizi ni kauli za kiongozi bungeni? Kauli ya Serikali? Kangi anahitaji kurudishwa shule asome lugha ya uongozi.

One comment

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.