Mapinduzi ya 1964 yaliua hata mapishi

TWAYIB! Imeingia Ramadhani na tupo barazani. Sijui kwanini Ramadhani hii inanikumbusha ya 1964  mwaka ulioiweka njia panda historia ya Zanzibar.  Mapinduzi yalikuwa bado mabichi, hayakutimu hata mwezi, ulipoandama mwezi wa mfungo wa Ramadhani.

Sizisahau siku hizo za mwanzomwanzo wa Mapinduzi. Kila jioni kukaribia kufungua mwadhini nikipanda baiskeli kuelekea jela ya Kiinua Miguu. Nilikuwa nikimpelekea futari  Sheikh Amor Zahor, jirani yetu aliyekuwa miongoni mwa wafungwa wa mwanzo wa kisiasa baada ya Mapinduzi.

Na Ahmed Rajab

Alikuwa baba wa Biubwa Amor, mfuasi wa Umma Party na mwanamke pekee wa Kizanzibari aliyekuwa akitembea na bunduki siku za mwanzo za Mapinduzi. Sheikh Amor alikuwa pia mkwe wa Ali Sultan Issa, mmoja wa viongozi wa Umma Party.

Yeye mwenyewe Sheikh Amor alikuwa miongoni mwa viongozi wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (maarufu kwa jina la Hizbu).  Alifungwa akafunguliwa halafu akakamatwa tena na akawa mmoja wa wazalendo wa mwanzo waliodhulumiwa roho zao mwaka huohuo wa 1964.

Ninawakumbuka askari wa Tanganyika walioletwa Unguja baada ya Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, kumuomba Rais Julius Nyerere wa Tanganyika amletee askari kusaidia kuimarisha amani na utulivu. Karume akiwahitaji askari hao pia wawe kama kinga ya kuzuia asipinduliwe.

Nyerere baadaye alitishia kuwaondoa askari wake katika njama za kumshinikiza Karume aukubali Muungano.

Imenijia hamu ya kuzichakurachakura kumbukumbu za utotoni nikivikata akilini mwangu vichochoro vya Mji Mkongwe nilikozaliwa na kukulia. Bado zinanijia harufu na sauti zilizokuwa zikihanikiza.

Ukisikia mlio wa vikombe vya kahawa ukijua tu huyo ni Karama au Awadh au “Bwan” Salim anayeinadi kahawa yake kwa mlio mahsusi wa vikombe vyake.

Mlio huo ukisababishwa na namna muuza kahawa akiwa na dele la kahawa mkono mmoja, alivyokuwa akivichezesha vikombe vya kahawa kwa vidole vya mkono wake wa pili.

Kuna mengi yaliyobadilika Mji Mkongwe. Mfano ni hao wauza kahawa waliokuwa wakiranda mitaani na madele yao ya kahawa kutafuta washtiri. Wala hawaonekani tena wauza maziwa wakiendesha baiskeli zao nyuma wakiwa wamepakia matangi ya maziwa.

Walikuwa wakitumwa kuyauza maziwa ya wenye maziwa. Wauza maziwa wa mjini karibu wote walikuwa na ng’ombe na mabanda yao yalikuwa eneo la Marhubi.  Baadhi yao wakifuga ng’ombe wao mashambani, kama babake Inspekta Ramesh Misra, Ramji China,  Baniyani aliyekuwa akiishi Mkunazini karibu na ilipo hoteli ya Luqman.  (Kwetu Zanzibar, hoteli huitwa hoteli lakini mikahawa kama Luqman au “Passing Show” nayo pia huitwa hoteli.)

Ng’ombe wakiagizwa kutoka Kenya na wakiwekwa karantini Mpigaduri baada ya kuteremshwa melini.

Siku hizo biashara kubwa ya maziwa ikifanywa na Wazanzibari wenye asili za kigeni na wa mjini kama hao Wahindi kina Ramji China.  Jamii mashambani walikuwa wafugaji wadogo.  Wengi wao wakiishi karibu na Mjini, wakileta matangi yao  juu ya baiskeli marikiti ya mboga  kukaguliwa na idara ya kilimo halafu wakifungiwa madumu kabla ya kuwauzia bidhaa yao kwa wateja.

Na alikuwako Sharif Maziwa (mjomba wake Profesa Ibrahim Noor Sharif) katika eneo la Shangani.  Kwa Sharif Maziwa kuko lakini wenyewe hawako. Hakuuzwi tena maziwa. Wenyewe wanakula raha, au kama tusemavyo wanakula unyunyu, kwingine kwa vile Mapinduzi yamewakimbiza.

Siku zile Mchambawima ndiko kulikokuwa kukiuzwa maziwa mengi.  Mchambawima nako kuko lakini mengi yaliyokuwako huko hayako.

Bibi yangu mzaa mama akitaka nitie mwili kwa hivyo alikuwa na dasturi ya kunipeleka Kizingo kuogelea pwani alfajiri na baadaye akinipeleka Mchambawima, karibu na markiti ya mboga, kwenda kunywa gilasi ya maziwa ya moto katika moja ya maduka ya maziwa yaliyokuwapo kwenye jumba lililokuwa la Mzee Boga.

Takriban milango yote ikiuza maziwa. Wa kwanza na uliokuwa mkubwa ulikuwa wa Madhani, Muismaili aliyekuwa pia dalali wa gazeti la Daily Nation la Kenya.

Maduka mingine yalikuwa ya Wahindi, jamii ya Makumbaro. Mawili ya kati yalikuwa ya familia ya Haji Omar Madhapuria na nduguze Essak na Yakub. Mimi nikipelekwa kwa Madhapuria ambako ndani mlikuwa na meza ndogo. Wachezaji maarufu wa soka wa timu ya Vikokotoni kina Abdul Majham na Shioni Mzee wakenda huko kunywa maziwa baada ya mechi. Watoto wengine wakenda kununua malai kwa pesa nne.

Wamiliki wa ng’ombe walikwenda kapa kwani mabanda yao yote ya ng’ombe ya Marhubi yalivamiwa na wapinduzi.

Wengi wa wafugaji wa ng’ombe na wauzaji maziwa walikuwa Makumbaro waliokuwa wakiishi karibu na markiti.  Walianza kwa biashara ya mbuzi.  Wengine walikuwa ni Maagha. Watu wengi huwaita Mabaharani, yaani Wazanzibari wenye asili ya Bahrain. Lakini kwa hakika, mababu zao walitokea Iraq.

Baadhi ya mabinti zao ndio walioolewa kwa nguvu kwa amri ya Serikali ya Mapinduzi na kuiaibisha nchi yetu mbele ya macho ya ulimwengu.

Nadhani moja ya dosari zinazoizuia Vatikani, makao makuu ya Papa, yamfanye Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu ni aibu hiyo iliyotokea alipokuwa Rais wa Tanzania. Alishindwa kuzizuia au hata kuzilaani ndoa hizo za haramu.

Madhani na Madhapuria waliendelea na biashara ya maziwa mpaka siku za Mapinduzi. Baada ya hapo wafanyakazi wao waliwatafuna na biashara yao ikafa.

Mabadiliko ya tabianchi, ukame na upungufu wa mashamba karibu na mji, yote hayo yalichangia kuzidi kuiua biashara hiyo iliyokuwa ikistawi Mchambawima.

Usiniulize nani aliyekuwa akichamba wima hata eneo hilo likabandikwa jina hilo.

Vichochoro viwili vitatu kutoka hapo unaelekea upande wa pili wa markiti kwa kina Abdulrahman Mohamed Hamdani maarufu kwa jina la Abdulrahman “Guy”, mwanzilishi wa Chama cha Kikomunisti cha Zanzibar ambako nilikuwa na mazoea ya kupitapita kusoma magazeti ya bure. Siku za mfungo wa Ramadhani vichochoro vyote hivyo vikinukia maandazi au maandalizi mengine ya futari.

Mapinduzi yamepindua mengi yakiwa pamoja na utamaduni wa vyakula.

Sitoshangaa endapo wazee wenzangu watatamani ujana wao urudi ili waushtakie masaibu yaliyowafika uzeeni.

Si hasha wanatamani, kama mimi, irudi mikate ya mofa, ya manda na ya ana. Hii mikate ya ana ilikuwa ya duara kama mikate ya ufuta lakini ilikuwa haitiwi ufuta, ilikuwa minene zaidi na ikitiwa sukari kwa mbali hivi.

Katika zungukazunguka zangu nimeikuta mikate ya mofa ikiuzwa Mombasa, Kenya, kwenye mkahawa wa Barke kule Kibokoni.Ya manda, yenye kupikwa kwenye majani ya mgomba, nimeikuta Comoro ambako inaitwa “mikate ya bwan tamu” lakini ladha yake tofauti kidogo na ile tuliyoizoea Unguja.

Zamani karibu hoteli zote (mikahawa) zikimilikiwa na Mahadhrami, watu wenye asili ya Yemen kutoka Hadhramout, ingawa Zanzibar wote huitwa Washihiri. Wakipika chai kwa maziwa ya mkebe na vyakula walivyokuwa wakiviuza vilikuwa vya ladha.

Ukiweza kununua kaimati, visheti, bokoboko, vyakula vya nazi, mikate ya mofa na ya ufuta, ingawa mimi udogoni mwangu nikitumwa kununua mikate ya ufuta darini juu kabisa kwenye jumba la Bwana Burhan al Amawi hapo Mkunazini karibu na Msikiti wa Memon. Mikate ya huko ilikuwa laini kama sufi na ikiyayuka mdomoni.

Nazikumbuka legeni za kuokea mikate ya kumimina. Siku hizo mikate ya kusukuma ilikuwa mikate ya kusukuma tu. Haikuwa na majina mbadala ya chapati au parata. Vipopopoo vilikuwa vipopoo na si matobosha.

Zama zetu vyakula vilivyopikwa vikapikika, kwenye maseredani na majiko ya kuni, vilikuwa mfano wa  nyimbo za taarab – vilijaa hisia mbalimbali.

Ukistarehe kula maandazi yaliyotiwa hiliki na arki ya vanilla ili yawe na harufu nzuri na ladha zaidi. Leo wapi! Labda upikiwe majumbani kwa jamaa wa mjini. Na hata huko kuna mengi yanayokosekana kama samli ya Kismayu ambayo siku hizi imepotea.

Siku hizi mengi yameharibika. Ubora wa vyakula mahotelini umeanguka. Wapishi hawana fahari na mapishi yao. Wanavifanyia uchoyo viungo kwa sababu bei  zimekuwa ghali.

Jioni karibu na msikiti Ruta kwa Mzee Khamis tukinunua sambusa na kuku wa kuchoma wa Abdillahi. Tukinunua sharubati za kila aina lakini tukitaka maji ya machungwa au ya ukwaju tukikimbilia kwa Khamis Machungwa, mishikaki ya urojo tukiipata karibu na sinema ya Majestic, mikate ya Ajemi kwenye hoteli moja ya Wahindi iliyokuwa marikiti, na haluwa Mtendeni kwa Mahruki.

Upande wa mwisho wa Sokomuhogo mtaa niliozaliwa karibu na kwa Adnani muuza mbatata za urojo, kulikuwa kukiuzwa tende kwenye duka la kina mwanaharakati Fatma Aloo. Na wao wakinunua nyuzi na nyaya za shaba na vinginevyo hata kutoka kwa watoto.

Jamaa yake Profesa Abdulaziz Lodhi, Haji Omar Essak akipika haluwa ya lozi na tamu tamu za kihindi kama ladu, nankhatai (nangatai) na biskuti za siagi.

Wengi wa wakazi wa leo wa mjini wametoka sehemu nyingine za Zanzibar na hawakuzoea mchanganyiko wa watu wa mjini wenye nasaba na tamaduni tofauti. Ni kinyume na ilivyokuwa zama zetu. Lakini tena kila kizazi kina mambo yake.

Kilichosalia cha zama zetu ni kumbukumbu za mazoea. Maisha yamekuwa magumu, bei za vitu ziko juu na mapato madogo,

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 8 Mei 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter:@ahmedrajab

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.