Kusitishwa Bagamoyo SEZ ni udhaifu wa uchumi na diplomasia

Serikali imetangaza bungeni kuwa mradi mkubwa wa Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (Bagamoyo SEZ) wa thamani ya dola bilioni 10 za Marekani (sawa na shilingi trilioni 23 za Kitanzania) umesitishwa na kuwa hautafanyika tena. Mradi huu mkubwa wa uwekezaji ambao thamani yake ni zaidi ya Bajeti ya Maendeleo ya Wizara nzima ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa miaka minne (TZS 18 Trilioni) haupaswi kufutwa tu bila mjadala wa kina. Ni lengo la makala haya kuibua mjadala huo.

Kwangu kufutwa kwa mradi wa Bagamoyo SEZ ni kielelezo cha uelewa mdogo wa Uchumi na Diplomasia uliotamalaki miongoni mwa watawala wa sasa wa nchi yetu Tanzania. Kwanza ni muhimu kuuelewa mradi wenyewe kabla ya kubomoa hoja za Serikali zilizotumika kufuta mradi huu. Watanzania wanapaswa kutambua kuwa mradi huu ni wa Uwekezaji kutoka nchi mbili ambazo tuna historia nazo kubwa, Oman na China, hivyo tutazama athari za maamuzi haya ya Serikali pia katika eneo hilo la mahusiano na nchi hizi mbili.

Kiujumla, Watanzania wengi wakisikia mradi wa Bagamoyo SEZ wanajua ni ujenzi wa bandari ya Bagamoyo tu. La si hivyo. Bandari ni sehemu tu ya mradi. Lakini Bagamoyo SEZ ni mradi wenye lengo la kuufanya mji wa kihistoria wa Bagamoyo kuwa kituo kikubwa cha usafirishaji mizigo (Main Logistics Hub) katika bara zima la Afrika. Ni uwekezaji wa ubia (Joint Venture Investment) kati ya wawekezaji kutoka China na Oman, ambao walikuwa tayari kuutekeleza kama Special Economic Zone (Eneo la Ukanda Maalum wa Uchumi Bagamoyo). Ujenzi wa bandari ni moja tu kati ya maeneo manne ya mradi huo mkubwa, maeneo mengine ya mradi ni pamoja na;

1. Ujenzi wa eneo la viwanda (industrial park) ambalo katika awamu ya kwanza litakuwa na viwanda 190 vitakavyozalisha ajira mpya za moja kwa moja 20,000 na awamu ya pili na tatu ikikamilika kutakuwa na viwanda 790 vitakavyozalisha ajira mpya 100,000.

2. Ujenzi wa mji wa kisasa wa makazi unaonendana na mahitaji ya karne ya 21. Ujenzi wa mji huu ulilenga kusaidia kupunguza msongamano wa jiji la Dar es saalaam kwani shughuli nyingi za uchumi zitakazotokana na Bagamoyo SEZ ungepelekea watu wengi kuhamia kwenye mji mpya kutoka Dar es Salaam.

3. Ujenzi wa kituo cha usafirishaji (Logistics Park) ambacho kingeifanya bagamoyo kuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo na hivyo kuiimarisha Tanzania kama njia kuu ya usafirishaji mizigo ‘transit route’ inayotoka na kuingia kwenda nchi mbalimbali tunazopakana nazo. Hii ‘Logistics Park’ ndio ililenga kuhudumia meli (handle transshipment) kutoka Afrika kwenda Ulaya na Marekani.

Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone

Mradi huu na maeneo yake hayo manne (4) ungekamilika, na haswa hilo eneo la nne (Logistics Hub), jumla ya kontena milioni 20 zilitarajiwa kupita Bagamoyo kwa mwaka na kuifanya kuwa bandari kubwa kuliko ile ya Rotterdam ya Uholanzi ambayo ndio kubwa kuliko zote bara la Ulaya. Kwa hakika, ndani ya miaka 10 Bagamoyo ingekuwa Dubai ya bara zima la Afrika.

Wazo la mradi huu linafanana na wazo la Mradi wa Shenzhen – Special Economic Zone, ambapo Kampuni inayotaka kuwekeza Bagamoyo ilikuwa mojawapo ya kampuni zilizowekeza huko. Ukanda Maalumu wa Uchumi wa Shenzhen ulikuwa Mpango Maalumu wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi ya China chini ya Kiongozi Deng Xiaoping.

Ulikuwa mji wa majaribio ya sera za kiuchumi ambazo zimeibadilisha nchi ya China na kuwa inavyoonekana sasa. Bagamoyo ilikuwa inajengwa kuwa Shenzhen ya Afrika kupitia mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone ambayo wengi hupenda kuita Bagamoyo Port kiufupi na kwa hakika kwa makosa.

Hii ndio bahati mbaya iliyotokea, watu wengi wanajikuta kuzungumzia bandari na huenda hata maamuzi ya kusitisha mradi yamefanyika kwa kuzingatia sehemu moja tu ya bandari na wameacha kufikiria manufaa makubwa ya ajira kutoka maeneo mengine matatu ya mradi, hasa kipindi hiki ambacho vijana wengi wa Tanzania wanamaliza shule bila matumaini ya kupata ajira rasmi au hata kujiajiri wenyewe.

Mradi huu mkubwa umekuwa gumzo sehemu mbalimbali ulimwenguni kutokana na ukubwa wake pamoja na athari zake kwa maslahi ya makundi mbalimbali ulimwenguni. Jambo moja muhimu sana kukumbukwa ni kuwa biashara ni vita vya makundi yenye maslahi mbalimbali. Rais John Pombe Magufuli amekuwa akihubiri kuwa nchi yetu ipo kwenye vita vya kiuchumi, masikini kwenye ‘The Bagamoyo Battle’ ameshindwa vita kabla hata risasi ya kwanza kupigwa. Maslahi yapo kutoka maeneo kadhaa:

1. Kwa mataifa ya Ulaya Magharibi, mradi huu ulikuwa tishio kwa hoja za kiushindani na ushawishi ndani ya ukanda wa Bahari ya Hindi ambao unabashiriwa kuwa kitovu muhimu katika bishara ya kimataifa katika miaka michache ijayo. Wazungu waliuona mradi huo kuwa utaipa China nguvu kubwa zaidi ya kiuchumi. Ilikuwa ni muhimu sana kwa wao kuhakikisha mradi huu hautekelezwi kwa namna yoyote ile ili kuzuia nguvu ya China katika ukanda huu.

2. Kwa mataifa mengine ya Afrika, mfano kwa SADC nchi kama Afrika ya Kusini – mradi huu ulikuwa tishio kwa maslahi yao ya kiuchumi kwa kuwa ungepelekea ushindani mkubwa kwa biashara ya bandari ya Durban ambako hivi sasa ndiko kuna bandari pekee zenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa kabisa za mizigo (4th generation ships). Inawezekana kabisa Afrika Kusini haikufanya kitu kuhujumu mradi huu, lakini kutofanyika kwake ni faida kubwa wa Durban, kwani Bagamoyo ilikuwa inakwenda kuwa mshindani wake mkuu. Hali ni hiyo hiyo kwa Angola ambayo inataka kujenga reli ya kuiunganisha DRC Kongo ili mizigo ya nchi hiyo ipitie bandari yao ya Luanda.

3. Kwa Afrika Mashariki, hasa Kenya, mradi wa Bagamoyo ulikuwa ni tishio kubwa kwa mradi wa bandari mpya wanayopanga kuijenga huko Lamu, ambayo nayo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa (4th generation ships) na pia itakuwa na kitovu cha usafirishaji wa mafuta barani Afrika. Siamini kuwa Kenya imefanya chochote kuhujumu mradi huu wa Bagamoyo SEZ, lakini maamuzi ya Tanzania kusitisha mradi huo yametoa ushindi wa bure bure kwa Kenya, kwani sasa meli kubwa zitahudumiwa Lamu na kuipa Kenya nafasi kubwa sana katika biashara ya usafirishaji katika eneo la Afrika Mashariki na Kati (The Great Lakes Region).

4. Taasisi nyingine za kimataifa zimeingia katika vita hivi kusaidia nchi zenye nguvu duniani. Benki ya Dunia (WB), kwa mfano, haikuupenda mradi huu na ni dhahiri kuwa imetumia ushawishi wake serikalini kuupiga vita Mradi wa Bagamoyo SEZ. Ushawishi huo uliwezekana kutokana na misaada na mikopo ambayo Benki ya Dunia inaipatia Tanzania na hivyo kupenyeza ushawishi wa kuupinga mradi. Hoja kubwa iliyotumika kupinga Mradi wa Bagamoyo ni kwamba kwa kuwa wao WB wameipa serikali mkopo wa maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, hivyo mradi wa Bagamoyo hauna tija, na endapo ungefanyika utaleta ushindani kwa Bandari ya Dar es salaam na hivyo kushindwa kulipa mkopo. Hoja hii ni muflisi, lakini serikali yetu ikaingia kingi na kupoteza Uwekezaji wa Fedha za Kigeni (FDI) wenye thamani ya USD 10 Bilioni (TZS 23 Trilioni) kwa tishio la mkopo wa USD 400 milioni (TZS 920 Bilioni). Inasikitisha sana!

Makundi hayo yote yalikuwa na maslahi yanayofanana ya kuhakikisha/kuombea kwamba Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone usitekelezwe. Maamuzi ya serikali yetu yamewezeshwa na matakwa ya makundi hayo, kwa kujua ama kutokujua. Najua kuwa imetumika nguvu kubwa ya ushawishi kwa kutumia propaganda za vyombo vya habari, ujasusi wa kiuchumi (economic intelligence) na hata ushawishi wa kisiasa (political influence and scaremongering).

Mfano ni kugonganisha utawala wa Awamu ya 5 na uongozi uliopita wa Awamu ya 4 (kwa kuonyesha kwa kuwa rais aliyepitisha mradi huu anatoka Mkoa wa Pwani, na hivyo amepeleka mradi huu kwao Bagamoyo kwa kujipendelea). Ndio maana kikao cha Baraza la Mawaziri, vikao vya mwanzo mwanzo tu vya utawala wa awamu ya tano, viliufuta mradi huu bila hata mjadala wa kina unaozingatia faida pana za mradi, na wala mahusiano ya kidiplomasia kati yetu na nchi za Oman na China.

Timu ya Tanzania ikiwa pamoja na wawakilishi wa Oman na China baada ya kusaini makubaliano ya awali ya mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone

Sasa tutazame hoja zinazotolewa dhidi ya mradi wa Bagamoyo SEZ ili kuona kama kuna mantiki:

1. Hofu ya serikali kupoteza mapato kutokana na ushindani wa Bandari ya Bagamoyo

Serikali imejengewa hofu kuwa Bandari ya Bagamoyo itafanya mapato ya Bandari ya Dar es Salaam kupungua na hivyo serikali kukosa mapato yake. Ukiangalia kwa juu juu hoja hiyo ina mantiki. Kwamba kutakuwa na ushindani na Dar es Salaam itapoteza mapato. Lakini yapo mambo matatu yanayothibitisha kwamba hoja hiyo sio sahihi:

Mosi: Bandari ya Bagamoyo itahudumua meli kubwa (4th generation ships) ambazo hivi sasa haziwezi kuingia katika Bandari ya Dar es Salaam. Katika biashara ya kimataifa hivi sasa, usafirishaji kwa kutumia meli kubwa ndio wenye tija, unafuu na faida. Kwa mfano, leo hii kusafirisha zao la korosho kutoka Tanzania hadi China au Marekani kwa kutumia meli ndogo inagharimu mara mbili ya gharama ya usafirishaji kwa meli kubwa.

Kutokuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa kumefanya gharama za usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi zetu kwenda kwenye masoko mengineyo kuwa kubwa na ghali mno (uncompetitive). Ndio maana leo hii nchi za Amerika Kusini, ambazo zipo mbali kabisa na China, zinauza bidhaa zake nyingi katika soko la China kuliko nchi za Afrika ambazo zipo karibu na China kijiografia.

Mfano halisi umetokea karibuni tu. Marekani ilipoanza vita ya biashara na China kwa kuongeza kodi katika bidhaa za China, ili kujibu mapigo, China nao waliongeza kodi kwa maharage ya soya kutoka nchini Marekani. Ikumbukwe kwamba biashara ya maharage ya soya ni kubwa sana kwa Marekani. Kila mwaka wanauza soya ya thamani ya USD 35 Billioni na zaidi kwa nchi mbalimbali, China ikinunua 60% ya soya yote.

Hivyo basi, kitendo cha China kuongeza kodi, gharama za soya zikapanda na hivyo wanunuzi wa soya kutoka China walitafuta soko mbadala la kununua soya (altenative source). Lakini badala ya kuja kununua Afrika, ambako ni karibu zaidi, waliamua kwenda kwa nchi za Amerika ya Kusini, hasa Brazili. Moja ya sababu ya kwenda kununua soya huko ni pamoja na uwepo wa bandari zenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa (4th generation ships) ambazo ni nafuu katika usafirishaji. Afrika imekosa fursa ya biashara kubwa sababu hiyo.

Pili: Uwepo wa bandari kubwa katika eneo moja unasaidia kuongeza wingi wa shughuli za usafirishaji wa mzigo kutoka kwenye bandari kubwa kwenda kwenye bandari ndogo, na hivyo kuongeza mnyororo wa thamani wa sekta ya usafirishaji. Mizigo mikubwa mikubwa ambayo ingeshushwa katika bandari ya Bagamoyo ingetengeneza fursa ya biashara kwa meli ndogo na za kati kuichukua Bagamoyo na kuipeleka kwenye bandari za jirani za Dar es Salaam, Tanga, Mombasa, na Beira. Mapato yangeongezeka badala ya kupotea.

Tatu: Ajira zitakuwa nyingi kwenye Bagamoyo SEZ kuliko kwenye upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam. Ni vizuri pia kujiuliza kuwa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam manufaa yake ni zaidi ya manufaa tutakayopata katika Mradi wote wa Bagamoyo SEZ? Hivi sasa Bandari ya Dar es Salaam inaajiri watu wangapi? Baada ya upanuzi utakaofanywa ni ajira ngapi mpya zitaongezeka?

Ukweli ni kwamba kwa teknolojia za karne ya 21, shughuli za bandari nyingi ziko kidijitali (digitalized) sana kiasi kwamba ile asili ya kuzalisha ajira nyingi haipo tena. Hivyo, kwa vyovyote vile, ajira mpya zitakazozalishwa baada ya kumalizika upanuzi hazitozidi 1,000. Kwa upande mwingine, ajira zitakazozalishwa kwenye mradi wa Bagamoyo SEZ katika awamu ya kwanza tu ni 20,000. Je faida ipo wapi? Mapato ya kodi za wafanyakazi hao 20,000 tu yatazidi mara 10 mapato yote ya serikali kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Nne: Kwa upande wa mapato (direct revenues) kwa Bandari ya Dar es Salaam, serikali inapata kiasi gani? Kwa vyovyote vile, mapato ya jumla ambayo serikali itayapata katika Mradi wa Bagamoyo SEZ yatakuwa ni makubwa zaidi, kwani mbali na mapato itakayoyapata katika eneo la bandari tu kwa njia ya tozo za mizigo na ushuru wa mizigo kwa bidhaa nyingi zitakazopitia katika bandari hiyo, serikali pia itapata kodi za aina mbalimbali katika viwanda 190 na baadaye viwanda 790 vitakavyojengwa.

Watumishi 20,000, PAYE yao itakuwa ni kiasi kikubwa cha uhakika kwa serikali. Achilia mbali shughuli mbalimbali za uzalishaji kutokana zitokanazo na shughuli za viwanda. Katika mji mpya utakaojengwa, serikali itapata kodi za majengo na kodi nyingine zitokanazo na ardhi na pango, achilia mbali kodi za shughuli nyingine za biashara zitakazofanyika Bagamoyo. Hoja ya mapato kupotea ni hoja dhaifu na haina mashiko kabisa.

Mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone

2. Hofu ya Mgeni Kuendesha Bandari

Hoja nyingine inayotolewa ni kwamba kumpa mwekezaji mgeni aendeshe bandari ni hatari kwa usalama wa nchi. Hapa cha kujiuliza ni kuwa ndani ya Bandari ya Dar es Salaam kuna kampuni ya Uwekezaji ya Kigeni, TICTS, ambayo imeendesha shughuli zake ndani ya bandari kwa miaka 20 na zaidi sasa, je ni usalama upi wa nchi umeathirika?

Inapokuja hoja za kiusalama ni nchi ya China yenye mahusiano ya karibu sana ya kijeshi na Tanzania. Kila leo tumeona vikifunguliwa vyuo (Chuo cha Ulinzi cha Jeshi Kunduchi), viwanja vya ndege (Uwanja wa Ndege wa Kijeshi wa Ngerengere, Morogoro), na kadhalika, kwa msaada wa China. Wanajeshi wengi wa Tanzania wamepata mafunzo China, na vifaa vingi vya kivita vimetoka China. Ni jambo la kawaida kukuta gari yenye namba za usajili za JWTZ ndani yake kuna askari wa Tanzania na China.

Sasa kwa ukaribu huo wa kihistoria tangu JWTZ ilipoanzishwa baada ya kuvunja jeshi lenye asili ya kikoloni lililojaribu kufanya mapinduzi miaka ya 60, leo hii sisi ndio watu wa kuhofia usalama dhidi ya Wachina? Hata hivyo, kama hoja hii ni ya kweli, je vyombo vyetu vya ulinzi na usalama haviwezi kuweka mkakati mbadala wa kudhibiti masuala ya usalama katika eneo la Mradi la Bagamoyo SEZ?

3. Hofu ya China kuchukua Mali za Taifa kama Zambia na Sri Lanka

Hoja nyingine inayozungushwa ni kwamba eti Wachina watanyang’anya mali za taifa endapo mradi huo utapata hasara kama ilivyokuwa kwa mradi wa Bandari wa Sri Lanka. Ukweli ni kwamba Mradi wa Bagamoyo sio sawa na mradi wa Sri Lanka au mradi wa ujenzi wa Reli ya Kenya. Tofauti na miradi hiyo miwili ya Kenya na Sri Lanka, Mradi wa Bagamoyo unatekelezwa kwa njia ya uwekezaji (FDI) kwa asilimia 100, wakati ile miradi ya Kenya na Sri Lanka inatekelezwa kwa mikopo ambayo nchi inawajibu wa kuweka dhamana (sovereign guarantee).

Hii maana yake maana yake ni nini? Hata kama Mradi wa Bagamoyo utaendeshwa kwa hasara, atakayeumia ni mwekezaji na sio nchi yetu. Lakini kwa uzoefu wa kampuni ya China Merchant katika uwekezaji wa miradi mikubwa ya aina hii, haiwezekani wakafanya uamuzi wa kuwekeza mradi wa kupata hasara kirahisi namna hiyo. Ikumbukwe kwamba kampuni ya China Merchant ina uwezo wake kimtaji unaofikia mara 20 ya pato la ndani (GDP) la Tanzania. Yaani mapato ya kampuni hiyo kwa mwaka ni USD 1,200 Bilioni, wakati GDP ya Tanzania ni USD 55 Bilioni.

4. Masharti Magumu

Hoja nyingine inayosemwa ni kuwa masharti ya kuendesha Mradi wa Bagamoyo ni magumu. Inawezekana kuwa hoja hii ina mashiko na ndio maana ni hoja pekee ambayo serikali inaitaja. Hata Bungeni ndio hoja ambayo Waziri wa Uchukuzi ameizungumza katika hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka 2019/2020.

Lakini tuulizane, hivi mahala ambapo watu wanazungumza, si kila upande una wajibu wa kuja na mapendekezo yake (proposals) na upande wa pili una haki ya kuja na yake (counter proposals)? Kuweka mpira kwapani sio njia sahihi hata kidogo, ni udhaifu uliopitiliza.

Kama serikali iliweza kwenda hatua ya ziada kuvutia mradi wa Bomba la Mafuta la Uganda kwa kutoa vivutio maalum vilivyopelekea hadi kufanyika mabadiliko ya sheria Bungeni, iweje ishindwe kufanya hivyo kwa Mradi wa Bagamoyo? Faida za ajira na kodi zinazokuja na Mradi wa Bagamoyo, kwa hakika zinazidi faida za Mradi wa Bomba la Mafuta ambalo sehemu kubwa ya ajira zake zitatokea wakati wa ujenzi wa bomba lenyewe na likishakamilika ajira zitapungua kwa 80%.

Ukiachilia faida za moja kwa moja zilizotajwa kuhusu Mradi wa Bagamoyo, ni wazi kwamba ujenzi wa mradi huo pia utasaidia kuufanya Mradi wa Reli ya Kati ya Standard Gauge kupata idadi kubwa ya mizigo ya kusafirisha ili uweze kurejesha mikopo iliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo. Serikali yetu inashindwa kuona fungamanisho hili kati ya Mradi wa Reli ya Kisasa na Mradi wa Bagamoyo SEZ? Kwa ujumla na vyovyote iwavyo, faida za mradi wa Bagamoyo SEZ ni kubwa kuliko madhara tunayodhani tunayaepuka.

Athari za Maamuzi Haya Kiuchumi na Kidplomasia

Inawezekana kuwa sababu zinazotajwa hadharani sio sababu haswa zilizopelekea Mradi wa Bagamoyo SEZ kusitishwa. Sababu zisizotajwa zinatamanisha kuzifahamu. Tuna wajibu wa kuzitafuta hizi sababu zisizotajwa. Kama zinazotajwa ndio sababu, basi si sababu maana hazina mashiko kulinganisha na faida kubwa za mradi huu kwa taifa, na hasa ajira na kwenye kukuza nafasi ya nchi katika dunia ya usafirishaji.

Utiaji saini wa mradi wa Bagamoyo Special Economic Zone

Nimalize kwa hoja ambayo sasa kama Tanzania tunapaswa kuwa nayo makini sana. Kwa miaka ya hivi karibuni nchi yetu imeanza kupoteza heshima yake kimataifa na hata kuelekea kupoteza marafiki wa kudumu (all weather friends). China na Oman, nchi ambazo zilikuwa zishirikiane na Tanzania kwenye mradi wa Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo (Bagamoyo SEZ) ni nchi muhimu sana kwa historia ya Tanzania.

China ilipoanzisha mikutano na Afrika (FOCAC) mwaka 2000 ni nchi 4 tu za Afrika zilihudhuria ikiwemo Tanzania. Hivi sasa FOCAC inahudhuriwa na marais wengi zaidi kuliko Mkutano wa AU wa kila nusu mwaka. Rais John Magufuli hajahudhuria mkutano hata mkutano mmoja wa FOCAC tangu aingie madarakani na hivyo kutoonana na Rais wa China kuzungumzia masuala ya maendeleo ya nchi zetu hizi. Mradi wa Bagamoyo ulikuwa mradi muhimu mno kwa wazo la Rais wa China la ‘Belt and Road Initiative’. Kutofanikiwa kwa mradi huu ni udhaifu wa kidiplomasia wa nchi yetu na udhaifu huu una gharama kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mshirika mwengine wa mradi huu ni nchi ya Oman. Oman ina historia kubwa kwa Tanzania na hususan Zanzibar. Katika raia takribani milioni 5 wanaoishi Oman, takribani nusu yake wanaongea kiswahili. Kama kuna nchi ambayo Tanzania inapaswa kuwa na mahusiano nayo ya karibu zaidi nje ya Afrika ni Oman. Hivi karibuni Oman imekuwa ikijitahidi kuimarisha mahusiano yake na Afrika Mashariki na Mradi wa Bagamoyo ilikuwa ni moja ya miradi ya kuonyesha nia na dhamira ya dhati ya Serikali ya Oman kuboresha mahusiano na Tanzania.

Oman inaagiza takribani vyakula vyote kutoka nje, na Tanzania ingeweza kufaidika sana na soko la Oman kwa bidhaa za kilimo na mifugo. Hivi sasa nchi zinazofaidika ni India na Sri Lanka. Mradi wa Bagamoyo ulikuwa mradi muhimu sana kuifungua Oman kwa Tanzania. Kutofanikiwa kwa mradi huu ni udhaifu wa kidiplomasia wa nchi yetu na udhaifu huu una gharama kubwa kwa maendeleo ya nchi yetu kiuchumi, hasa kwa wakulima na wafugaji.

Jambo linalonishangaza kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano ni uwezo wake wa kukumbatia miradi inayotoa fedha nje (outflows) na kuua miradi yote iliyoikuta ya kuleta fedha nchini (inflows). Mradi wa kinu Cha kuchakata Gesi Asilia cha Lindi (LNG) wenye thamani ya USD 30 bilioni (TZS 69 Trilioni) umecheleweshwa, Mradi wa Uwekezaji kwenye Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Liganga wenye thamani ya USD 3.5 Bilioni (TZS 8.05 Trilioni) nao pia umecheleweshwa, na sasa Mradi wa Ujenzi wa Ukanda Maalumu wa Kiuchumi wa Bagamoyo kuifanya Tanzania kuwa Kituo Kikuu Cha Usafirishaji Afrika nzima, wenye thamani ya USD 10 Bilioni nao umesitishwa.

Utekelezaji wa miradi hii mitatu ungerahisisha sana utekelezaji wa miradi ambayo Serikali inafanya sasa. Mradi wa LNG ya Lindi ungeipa nchi mabilioni ya fedha za kigeni kutekeleza mradi wake pendwa wa Stiegler’s Gorge kama ingekuwa kuna haja kuendelea nao. Mradi wa Mchuchuma na Liganga ungewezesha kuzalisha mataruma ya reli hapa hapa nchini kujengea reli ya SGR na kuokoa mabilioni ya fedha za kigeni tunayotumia kununulia mataruma nje ya nchi. Mradi wa Bagamoyo ungeleta mizigo yote ya Afrika hapa Tanzania na reli mpya kupata biashara na hivyo kupata faida ya uwekezaji.

Iweje sasa maamuzi yawe kuchelewesha na kufyeka miradi muhimu kama hii? Hakika sina majibu ya maamuzi ya namna hii, ila najua ni maamuzi ya hovyo yasiyo na faida kwa taifa letu.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Zitto Kabwe – kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini – akishirikiana na mtu mwengine ambaye hakumtaja jina kupitia mtandao wake wa Facebook tarehe 13 Mei 2019. 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.