Tanzania yahitaji mitume ili viongozi waheshimu katiba

NOVEMBA 27, 2015, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi aliliambia Bunge la India, chemba ya chini (Lok Sabha) kuwa misingi ya uasisi wa Taifa ilikuwa dini ya Serikali ni “India kwanza” na Katiba ndiyo kitabu kitakatifu kwa nchi.

Hotuba ya Modi ilikuwa sehemu ya kuadhimisha mwaka wa 125 wa kuzaliwa mmoja wa waasisi wa India na mwenyekiti wa kamati iliyoandika Katiba ya Taifa hilo, Dk Bhimrao Ambedkar ambaye huitwa Babasaheb, yaani “baba wa heshima” kwa lugha za Hindi na Marathi.

Na Luqman Maloto

Nimevutiwa na maneno hayo, kwamba dini ya Serikali ni “India kwanza” na kitabu kitakatifu ni “Katiba”. Maneno yasipoishia tu mdomoni na kuyeyukia masikioni, yakafika moyoni na kutuama, hapo nchi na watu wake ni salama mno.

Serikali ya Tanzania inahitaji kuuishi msingi huu; dini ya Serikali ni “Tanzania kwanza” na kitabu kitakatifu cha nchi ni “Katiba”. Tanzania ni nchi isiyofungamana dini yoyote, kwa maana ya mapokeo ya kiimani kuhusu Mungu, utaratibu wa kuishi na kuabudu.

Hata hivyo, baada ya dini hizo za thiolojia, nchi inapaswa kuwa na dini moja yenye kuwaunganisha watu wa dini zote na hata wapagani. Dini hiyo ni Tanzania kwanza. Dini za thiolojia zina vitabu vitakatifu. Kitabu kitakatifu cha dini ya nchi ni Katiba.

Ufafanuzi; dini ya nchi kama ilivyotamkwa na Modi, shabaha yake si kuwafanya watu wafaulu uzima wa milele baada ya kifo, bali kuwaunganisha watu kuwa jamii moja. Utakatifu wa Katiba haumaanishi ukitii yaliyoandikwa na kuyaishi ndiyo utaenda peponi, isipokuwa utakuwa mtu bora kwenye nchi.

Hekima za Modi kuitamka India kwanza ndiyo dini ya India na Katiba kama kitabu kitakatifu, zinashabihiana na falsafa ya Political Religion, kwa maana ya Siasa za Dini.

Nadharia ya Siasa za Dini maana yake ni Serikali yenye nguvu kitamaduni na kisiasa kwa wananchi, sawa na imani za kidini. Hapa inadhihirisha jinsi ambavyo Sayansi ya Siasa inavyotambua nguvu ya dini kwenye nchi.

Uchambuzi wa nadharia hiyo ni kwamba Serikali ambayo inaweza kujenga ushawishi kwenye maisha yao ya ndani kabisa kwa kuoanisha siasa na tamaduni zao, ndiyo ambayo hupata mafanikio yenye kushabihiana na imani ya kidini kwa watu.

Somo la Unyenyekevu

Dini zinafundisha unyenyekevu kwa Mungu. Kumwabudu na kutii maagizo yake ndani ya vitabu vitakatifu. Katiba inaelekeza utu, usawa na haki kwa kila mwananchi

Dini za thiolojia zimefanikiwa sana. Japo maovu yapo lakini angalau inafahamika kuwa kuna dhambi na thawabu. Watu wanakwenda misikitini na kanisani. Viongozi wa kiroho wanaonya maovu na kuelekeza matendo yaliyo mema.

Dini za thiolojia zimezama kwenye kina kirefu mno ndani ya mioyo ya watu. Unaweza kumchezea kwingine lakini si kwenye imani yake. Inaelekezwa kwamba ni hatari mno kuingiza chokochoko za udini kwenye nchi. Vita yake ni mbaya.

Inatakiwa ule unyenyekevu wa watu kwenye dini zao, wawe nao pia kwa nchi yao. Wawe watiifu kwa Katiba. Wakifahamu kuwa Katiba haiwapeleki mbinguni, ila maelekezo yake ndiyo yanawezesha watu kuishi na kuabudu vizuri kupitia dini zao. Kumbe Katiba ni njia pia ya kumfikia Mungu.

Katiba isipoheshimiwa inaweza kuzaa machafuko kwenye nchi. Eneo lenye machafuko ni vigumu kufanya ibada, maana watu huwa roho juu. Mauaji ya Kimbari Rwanda mwaka 1994, watu waliokimbilia kanisani kuokoa maisha yao waliuawa.

Kuna viongozi wa makanisa walikutwa na hatia kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu Arusha, kwamba waliwafungia ndani watu waliokimbilia makanisani ili wauawe. Hivyo basi, Katiba ikichezewa. Machafuko yakitokea. Ufalme wa Mungu unakuwa mbali, kwani fursa za kuabudu huadimika kama si kutoweka.

Nini Kifanyike?

Mpaka hapa kuna jambo ambalo haliwezi kubishaniwa. Hilo ni Katiba. Kwamba inapaswa kulindwa na kutetewa ili nchi iwe salama. Lingine lisilobishaniwa ni kuwa watu wanaamini dini zao na vitabu vyao vitakatifu. Wananyenyekea mno kuliko unyenyekevu wao kwenye Katiba.

Muhimu kuwausia watu waendelee kuwa waaminifu kwenye imani zao. Wamche Mungu. Hata hivyo, nchi inahitaji maarifa, namna ya kufundisha Katiba na Utaifa ili kuwajengea watu imani na unyenyekevu kama dini zao.

Kama Kanisa linavyoeneza Injili au Msikiti unavyotetea Kuran, ndivyo nchi inatakiwa kwa Katiba. Ikibidi kuwepo na somo la imani kuhusu Katiba. Kama ambavyo mtu akiipinga Injili anakuwa ameukataa Ukristo na mwenye kuikataa Kuran anatamkwa kafiri, ndivyo mvunjaji wa Katiba anatakiwa kuonekana ameukataa Utanzania.

Awe kiongozi au raia yeyote kwenye nchi, akifanya jambo lolote lenye kuvunja Katiba, anapaswa kuonekana ameukataa Utanzania. Yaani ameasi dini ya “Tanzania kwanza”. Kwa kuiga hukumu ya Uislamu, mvunja Katiba anapaswa kuitwa kafiri wa Utanzania.

Nchi inahitaji maarifa mapana kufundisha hili. Kama Yesu alivyoeneza Injili, Muhammad (S.A.W) alivyofundisha Kuran, Mussa na Torati au Daud na Zaburi. Je, walitumia njia gani kuwafanya wafuasi wao wawe wanyenyekevu na wenye imani zenye kina kirefu kuhusu dini na vitabu vyao vitakatifu?

Taifa likijifunza maarifa hayo ya mitume wa Mungu bila shaka elimu mahsusi itaenea. Mashuleni kuanzia chekechea watoto watafundishwa kuhusu Katiba na utakatifu wake. Wakiijua na kuishiba Katiba, watafahamu wajibu wa kuulinda Utaifa wao. Utanzania wao.

Nchi haitakuwa kama sasa Katiba inavunjwa na watu hawashtuki. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof Mussa Assad mwaka wa fedha 2017-2018, imeonesha jinsi fedha nyingi zilivyotumiwa kiholela na kwa kuvunja Katiba, lakini mwezi umepita kimya. Watanzania hawashtuki maandiko ya kitabu chao kitakatifu (Katiba) kupinduliwa. Imani kwa Katiba na Utaifa bado ni haba kwa Watanzania.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.