Msiba wa Mengi umewaumbua viongozi jeuri

“KWETU kweli kuna mambo. Lakini ya kwenu yamezidi, wala usikatae,” alinambia wiki iliyopita mwanasiasa mmoja mashuhuri wa Uganda. Simtaji jina asije akaanza kuninyima uhondo wa uchambuzi wake wa siasa za ukanda wa Afrika Mashariki.

Aliponambia aliyonambia nilijua akipiga wapi. Nimezoea kuisoma sauti yake iliyo nene kama asali nzito, au chambilecho rafiki yangu Chama Omari Matata wa shirika la utangazaji la BBC anayeiita sauti kama hiyo “sauti ya siagi”.

Na Ahmed Rajab

Matamshi yake yalikuwa ya mkato na ya fumbo lakini nikijua kwamba akiyazungumzia “manyago” ya wanasiasa wa Tanzania wakati wa msiba wa Dkt. Reginald Mengi, aliyekuwa mmiliki na mwenyekiti wa kampuni zilizo chini ya mwavuli wa Kundi la Kampuni za IPP na aliyefariki ghafla Dubai Mei 2 mwaka huu.

Mengi alikuwa mmoja wa matajiri wakubwa wa Tanzania. Jarida la fedha la Forbes lilikisia mwaka 2014 kwamba  alikuwa na utajiri uliopindukia dola za Marekani milioni 560. Pamoja na hayo alikuwa pengine mjasiriamali aliyejulikana zaidi nchini mwake kushinda wafanyabiashara wenzake.

Pia alikuwa mjomba wa Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kuitaja alaka yake na Mbowe si kusema kwamba alikuwa mpinzani. Nijuavyo ni kwamba alikuwa na uhusiano mwema na Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichokuwa akikifadhili chini kwa chini. Matajiri wengi wa Tanzania huwa wakicheza huku na huku.

CCM sio tena chama kinachowavutia wafuasi kwa itikadi yake. Kimegeuka na kuwa taasisi ya kibiashara yenye kuwavutia wafanyabiashara wakubwa wakubwa.

Wasiojipeleka wenyewe, hufuatwa. Wanajua kwamba wasipojipendekeza kwa CCM huenda wakaziona biashara zao zinakwamishwakwamishwa.

Sikujaaliwa kumjua Mengi. Niliwahi kukutana naye mara moja tu. Ilikuwa Machi 18, 1999 jijini Johannesburg, Afrika Kusini, wakati wa sherehe ya kuwapa tuzo za CNN waandishi bora wa Kiafrika kwa mwaka 1998.

Nilikuwa katika jopo la majaji saba tulioteuliwa na kituo cha televisheni cha CNN kuamua ni wepi kati ya waandishi kutoka nchi 15 za Kiafrika wa magazeti, televisheni na redio waliostahiki kutunzwa kwa kazi zao.

Miongoni mwa majaji wenzangu walikuwa Mike Hanna ambaye siku hizi ni mwandishi wa New York wa kituo cha televisheni cha Al Jazeera na Joel Kibazo aliyekuwa mwandishi wa masoko wa gazeti la Financial Times la Uingereza na aliyekuwa mwenyekiti wa jopo letu.

Mshindi mkuu alikuwa Declan Okpalaeke wa gazeti la Guardian la Nigeria. Kulikuwa na washindi wane wengine kutoka Nigeria, wane kutoka Afrika Kusini, mmoja kutoka Liberia na mmoja kutoka Kenya, Linus ole Kaikai, wa shirika la utangazaji la KTN.

Washindi walikabidhiwa tuzo zao na Cyril Ramaphosa, Rais wa sasa wa Afrika Kusini. Siku hizo alikuwa mwenyekiti wa shirika la magazeti la Times Media Ltd., South Africa.

Miongoni mwa wafadhili waliochanga kugharimia hafla ya tukio hilo ilikuwa kampuni ya IPP ya Mengi. Hiyo ndiyo sababu iliyonikutanisha na naye katika ukumbi wa Civic Theatre, Johannesburg usiku huo wa Machi, 18, 1999.

Mazungumzo yetu hayakuwa ya muda mrefu lakini kwa muda niliozungumza naye nilitambua kwamba hakuwa mtu wa kawaida na kwamba alikuwa na shauku kubwa ya kuwanyanyua Watanzania wenzake wasiobahatika kama yeye.

Hata hivyo, nakumbuka kwamba nikihisi nilikuwa na mtu aliyekuwa kidogo kama ana wasiwasi na pengine aliyefikiri kama usiku ule alikuwa pahala pasipo pake. Hizo zilikuwa dhana zangu.

Nakumbuka pia nikijiuliza mwenyewe kwa mwenyewe ilikwendakwendaje mhasibu huyo akajichumia utajiri aliosemekana kuwa nao.  Alikuwa amekwishaanza kuvuma kwa nguvu kwamba alikuwa kwenye tabaka la mamilionea wazawa wa Tanzania.

Kuna waliokuwa wakivumisha kwamba utajiri wote huo haukuwa wake na kwamba alikuwa akiwalindia wenye mali zao.  Sasa tunajua kwamba uvumi huo ukivumishwa na wasiokuwa wakimtakia mema. Lazima wakimuoena choyo na husda. Utajiri aliokufa nao aliupata kwa jitihada na nguvu zake mwenyewe.

Inavyoonesha ni kwamba Mengi alikuwa mtu aliyekinai.  Alipoona amepata utajiri wa kumridhisha alijitolea kuwanyanyua wanyonge wenye kudhalilika na maisha. Ndio maana kifo chake kiliwagusa wengi nchini Tanzania na nje ya Tanzania kwa ukarimu wake, na hasa kwa shughuli zake za kuwasaidia walemavu.

Halikuwa jambo la kushangaza kwamba msiba wake uliwavutia watu wengi mno waliokwenda kumuaga wakionesha masikitiko yao kwa kuondokewa na mtu waliyempenda.

Lililoshangaza na kuzidi kuhuzunisha katika msiba huo ni viroja vya wanasiasa walioonekana kukosa adabu kwa kulumbana na kusutana katika tukio hilo la maombolezi lililokuwa liwe la hishima na intidhamu.

Badala yake walipageuza pa msibani  pawe uwanja wa siasa, tena si siasa za kiungwana bali za kuchafuana.  Ilikuwa aibu si aibu, fedhedha si fedheha, izara tupu.

Taifa liliwashuhudia katibu mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ali na Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, wakijikashif.  Ilisikitisha kuwaona wanasiasa wa hicho chama kikongwe wakiziingiza siasa pasipostahiki. Na siasa zenyewe zilikuwa za kitoto si za kijitu uzima.

Hayo ndiyo yaliyomfanya yule mwanasiasa wa Uganda niliyemdhukuru mwanzoni mwa makala haya aione Tanzania kuwa ni nchi iliyoipiku nchi yake kwa viroja vya kisiasa. Tulipokuwa tunaendelea na mazungumzo yetu tulianza kuodhoresha maovu yanayofanywa na watawala wa Tanzania.

Tulipomaliza tulijikuta na orodha refu ya visa vingi vya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizwaji wa wananchi. Miongoni mwa visa hivyo ni kubanwa kwa uhuru wa kuikosoa serikali na wakuu wake, uhuru ambao ni haki wanayopewa Watanzania na katiba ya nchi.

Kuna yaliyomfika karibuni mwanachama wa upinzani Mdude Nyangali (maarufu Mdude Chadema) aliyetekwa na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha na wanaosemekana kuwa watu wa usalama wa taifa. Kampeni kubwa ilianzishwa mitandaoni Tanzania na Kenya kutaka waliomteka wamuachie huru.

Hatimaye Mdude aliachiwa lakini baada ya kuteswa na kuumizwa vibaya.

Tangu 2017, Tanzania imekuwa ni nchi yenye “watu wasiojulikana” ambao kazi yao imekuwa kuteka wapinzani na kuwatesa. Mwanamuziki Roma Mkatoliki na wenzake wawili walitekwa na watu wasiojulikana na waliachiwa siku tatu baadaye. Hao ndio walionusurika.

Wengine, kama Ben Saanane, msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, ametekwa na amepotea. Hadi leo hajulikani alipo. Azory Gwanda, mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Ltd., alipotea Novemba 21, 2017 katika mazingira ya mazongezonge. Hadi leo hajulikani yuko wapi.

Daniel John, kiongozi wa Chadema, alitekwa wakati wa uchaguzi mdogo wa Kinondoni Februari 11, 2018. Maiti yake ilipatikana siku tatu baadaye. Aliuliwa kikatili.

“Watu wasiojulikana” waliazimia kumtoa roho na kummaliza Tundu Lissu, mbunge wa Chadema na mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni. Walimtwanga kwa risasi Septemba 7, 2017 huko Dodoma. Zake bado ziko na aliyakwepa mauti. Angaliko Ubelgiji anakotibiwa baada ya matibabu ya awali jijini Nairobi, Kenya.

Halafu kuna kadhia ya viongozi wa vuguvugu la Uamsho. Huu ni mwaka wa sita kuendea wa saba tangu wakamatwe Zanzibar kwa amri ya viongozi wa huko na kufungwa Bara kwa shutuma zisizoeleweka.

Walipokamatwa awali Zanzibar ilikuwa kwa shtaka la kuhujumu miundombinu wakati wa maandamano. Upande wa mashtaka ulidai kwamba waliitia hasara serikali ya Zanzibar ya takriban shilingi milioni 500.

Kwa mujibu wa sheria ya Zanzibar watuhumiwa wakiwekwa ndani kwa muda wa mwaka na upelelezi wa kesi yao usipokamilika lazima waachiwe huru kabisa au kwa dhamana. Ndipo walipoongezewa tuhuma ya ugaidi na wakapelekwa kufungwa Bara.  Kosa la ugaidi halina dhamana.

Kesi yao inazorota huku wakidhalilishwa gerezani na hadi sasa serikali imeshindwa kuwasilisha ushahidi utaothibitisha mashtaka yao Ni wazi kwamba wakubwa wameazimia viongozi hao waselelee jela..

Wengi wanaamini kwamba yamewakuta yaliyowakuta kwa sababu ya msimamo wao wa kuwaamsha wananchi wa Zanzibar kuhusu suala la Muungano na utetezi wao wa demokrasia ya dhati.

Hayasahauliki matamshi ya kibri na mikogo ya makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipouliza kwenye mkutano wa hadhara: “Wako wapi Uamsho?”  Akajijibu mwenyewe: “Wako Bara wananyea ndooni”.

Sifa moja waliyonayo watawala wa Zanzibar na wa Bara ni kibri. Imekuwa kama wameambukizana. Wananchi wanawaangalia huku wakifoka kwa ghadhabu.

Wana ghadhabu lakini pia wamejawa na matumaini.  Wanatiwa moyo na matokeo ya uchaguzi wa wiki iliyopita wa Afrika Kusini ingawa bado viongozi wa ANC wanashika hatamu za utawala.

Zaidi wanayadurusu matukio ya hivi karibuni katika Algeria na  Sudan. Wanaamini kwamba iko siku na wao pia watawaondoa watawala wao.

Hiyo si ndoto bali ni ahadi ambayo daima historia huwapa wenye kukandamizwa na kudhulumiwa haki zao.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 15 Mei 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com na au Twitter:@ahmedrajab

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.