Nilivyomjuwa Shamuhuna

Sikumjua Ali Juma Shamuhuna mapema ila hadi pale aliporudi kutoka Ulaya na nakumbuka pembeni watu wakimwita Reegan (Ronald Reegan alikuwa Rais wa Marekani) na yeye akiwa ndio kwanza anarudi kutoka huko masomoni.

Kimichezo nakumbuka alikuwa makini katika kuisimamia timu ya netiboli ya Kilimo na kukusanya nyota mbali mbali wa mchezo huo na timu hiyo kwa kweli ilitikisa sana katika rubaa za mchezo huo hapa Zanzibar na Tanzania Bara, na naamini pia ilicheza michuano ya Ubingwa wa Afrika Mashariki. Japo haikuwahi kuwa bingwa Tanzania.

Kwenye soka alijitokeza wazi wazi kuwa mpenzi na mfadhili wa Small Simba na siku hizo za miaka ya 1980 na 1990 Small Simba chini ya Abdulghani Msoma ikawa timu tishio sana na kutamba Zanzibar na Tanzania Bara hata katika kiwango cha Afrika Mashariki.

Ila nilijua mengi ya michezo kuhusu Shamhuna kuwa alikuwa mpiga chandimu mzuri sana katika viwanja vya soka vya Zanzibar katika miaka ya 1950 na 1960 na alikuwa katika ramani ya mtaalamu wa timu za vijana wa Zanzibar Marehemu Hija Saleh. Alikuwa akitakiwa na vilabu vyote vikubwa.

Siku hizo timu za vijana zilikuwa ni pamoja na Caltex, Fulham, New Moon na nyengine na zile kubwa zaidi maarufu zilikuwa Polisi, Kikwajuni, Malindi, Miembeni na Vikokotoni.

Pia Shamhuna alikuwa mchezaji gofu kwa kuanzia na caddy boy ( mbeba mikwaju ya gofu) na kwa hivyo alisuguana mabega na wachezaji maarufu wa wakati wake ambapo ikichezwa viwanja vya Maisara ambapo pakiitwa Coopers Ground, ambapo siku hizo kriketi na hoki pia ilikuwa michezo maarufu sana.

Cooperss Ground pia pana kumbukumbu nzuri ya Zanzibar kwa sababu ndipo Mkoloni wa Uingereza alipotolea uhuru wa Zanzibar Disemba 10,1963.

Upele ulipata mkunaji pale Shamuhuna alipokuja kuteuliwa kuwa Waziri wa Michezo nafasi ambayo alidumu kwa miaka mingi na moja ya alilofanikiwa ni kuwa kipindi chake Zanzibar ilishinda Kombe la Vijana la Afrika Mashariki U-19 pale 2003.

Mimi na Shamuhuna tulisadifu mkwaruzano mkubwa pale aliponishutumu kwa mitizamo yangu ya uandishi kwenye Baraza la Wawakilishi na mimi nikamtumia salamu kuwa nitatumia kalamu yangu kurudisha makombora kwa vile amenituhumu katika eneo ambalo mimi siwezi kuingia kujibu aliyoyadai.

Pia nilipingana nae juu ya sheria ziliozokuwa zinapita kwake kuminya uhuru wa vyombo vya habari.

Nilimtumia Bw Said Shaaban siku hizo Naibu Katibu Mkuu juu ya nia yangu hiyo na kwa bahati akaweza kutukutanisha Ukumbi wa Uwanja wa Amani VIP na suluhu baina yetu ikapatikana.

Kuanzia hapo tukawa suhuba kiasi ambapo alinichagua vipindi viwili vya miaka mitatu kila kimoja kuwa Mjumbe wa Baraza la Michezo chini ya Bi Shariffa Khamis na pia kipindi kimoja cha miaka miwili kuwa Mjumbe wa Bodi Chuo cha Uandishi wa Habari.

Kitu chengine cha kuhusu michezo alichonipa heshima Shamuhuna ni kufanya utafiti na kuandika barua ambayo ndio iliotumiwa na Serikali ya Zanzibar kwenda kuombea uanachama wa FIFA mwaka 2010. Pia nilipwa vyema kwa kazi hio.

Barua hio ikafikishwa kwa Sepp Blatter Rais wa FIFA na yeye Shamhuna akifuatana na Rais wa ZFA Ali Ferej, ambao wamepishana kwa kifo kwa siku moja.
Kwa ukaribu wetu wa kimichezo Marehemu Shamuhuna alikuwa kila mwaka ananialika Maulid ya Homu kwao Donge ambapo yeye alikuwa ni muumini wake mkubwa, lakini nilibahatika kwenda mara moja tu, na hapana shaka alifurahi sana

Ally Saleh Alberto

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.