Uchokozi wa kina Bolton hautofua dafu

JOHN Bolton si mtu wa kuchezewa.  Akiwa mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani ana ushawishi mkubwa kwa Rais wa Marekani.

Uzuri wake ni kwamba hayabanii yaliyo moyoni mwake.  Huyasema wazi, ukipenda au usipende kuyasikia.

Siku zote katika medani ya sera za Marekani, naziwe za uchumi au za siasa za nje, huwako watu wa aina mbili. Kuna wale waitwao “njiwa” na wale wanaoitwa “mwewe”.

Katika sera za mambo ya nje “njiwa” ni wale wenye kutetea amani na wenye kutaka pawepo uhusiano mwema baina ya Marekani na mataifa mingine.

Ahmed Rajab

Na Ahmed Rajab

“Mwewe” huwa ni wale wenye kutaka Marekani itumie nguvu za kijeshi katika siasa za nchi za nje.

Bolton ni mwewe.  Ni mtu hatari mwenye kuona raha Marekani ikitumia mabavu kuziangamiza nchi za wengine. Babake alikuwa askari mzimamoto lakini yeye, msomi aliyesomea sheria katika chuo kikuu maarufu cha Yale huko Marekani, inaonesha amejitolea kuwasha moto hasa katika nchi zenye mafuta. Kiitikadi yeye ni muhafidhina mamboleo ingawa mwenyewe anasema itikadi yake ni kuiweka Marekani mbele, yaani kutetea maslahi ya Marekani.

Mambo aliyoyafanya katika siasa za kimataifa si ya kiungwana.

Alipokuwa msaidizi wa mwanasheria mkuu wa serikali chini ya Rais Ronald Reagan alipinga vikali wasilipwe fidia Wamarekani wenye asili ya Japani waliokuwa wamezuiwa kwenye kambi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Tena Bolton ni fidhuli. Mwaka 2002 alimlazimisha José Bustani ajiuzulu kwenye wadhifa wake wa kuwa mkuu wa idara ya Umoja wa Mataifa yenye kuzuia silaha za kemikali.

Bustani, raia wa Brazil, alisema Bolton alimpa muda wa saa 24 ajiuzulu huku akimtisha kwa kumwambia: “Tunajua wapi watoto wako walipo.”

Amewahi kusema kwamba “hakuna Umoja wa Mataifa. Kuna jumuiya ya kimataifa ambayo mara moja moja huongozwa na dola pekee halisi lililobaki, yaani Marekani na kwa maslahi yetu na pale tunapozifanya nchi nyingine zituunge mkono.”

Kwa muda mrefu, Bolton amekuwa akiyapinga Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na amesisitiza kwamba Marekani haitoshirikiana nayo.

Septemba mwaka jana alitoa hotuba akiiambia ICC kwamba kwa Marekani mahakama hayo “ni maiti”.

Bolton alikuwa miongoni mwa waliopanga njama zilizompelekea Rais George Bush wa Marekani aivamie kijeshi Iraq 2003 kumpindua Saddam Hussein.

Baada ya Saddam na utawala wake kuporomoka Bolton, akaanza kuzikamia serikali za Cuba, Iran, Korea ya Kaskazini, Libya, Syria, Venezuela na Yemen. Amekuwa akitaka Marekani izipindue.

Yeye pia alikuwa mshika bendera wa ile safu ya wanasiasa wa Marekani waliokuwa wakishikilia kwamba nchi yao ijitoe kutoka mkataba wa nyuklia uliofikiwa na Iran pamoja na nchi tano zilizo wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (China, Marekani, Ufaransa, Uingereza na Urussi) pamoja na Ujerumani na Muungano wa Ulaya (EU).

Bolton alifanikiwa katika njama hiyo kwani mnamo Mei 8, 2018, Rais Donald Trump aliushangaza ulimwengu alipotangaza kwamba Marekani inajitoa kutoka kwenye mkataba huo na alitaka uvunjwe kabisa. Hilo la pili halikuwezekana kwa sababu Iran pamoja na mataifa mingine iliyotiliana nayo saini mkataba huo bado yanataka uendelee.

Bolton aliuanza ushari wake dhidi ya nchi asizozipenda tangu alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Alikuwa mshabiki mkubwa wa Vita vya Vietnam ingawa yeye mwenyewe alikwepa asipelekwe vitani.

Kwa muda Bolton amekuwa akitaka Marekani iishambulie Iran kwa dhamira ya kuupindua utawala wake wa Kiislamu.

Machi 26, 2015 aliandika makala kwenye gazeti la New York Times yaliyokuwa na kichwa cha maneno “Kulizuia Bomu la Iran, Ipige Bomu Iran”. Hayo yalikuwa makala ya uchokozi ya kuchochea vita na Iran.

Pia yalikuwa na uchochezi wa aina mbili nyingine ambao ulionekana kwa mbali: wa kidini na wa kikabila.  Ulikuwa uchochezi wa kuyagonganisha madhehebu ya Sunni na ya Shi’a na wa kuwagonganisha Waarabu na Waajemi.

Kisingizio chake kilikuwa kwamba Wasaudi, Waarabu ambao wengi wao ni Masunni hawatokubali kupitwa na Waajemi ambao wengi wao ni Mashi’a.

Hila ya kuwagawa watu ili wafarakane waweze kuwatawaliwa ni hila kongwe ya wakoloni na mabeberu. Ni moja ya mbinu wanazozitumia kutugawa sisi wa ulimwengu wa tatu tusiweze kuwa wamoja kupambana na uroho wao wa kuzipora maliasili za nchi zetu, mafuta yakiwa mojawapo ya mali hizo.

Inashangaza kuwasikia baadhi ya wanasiasa wetu wa Kiafrika wakipata taabu kufahamu kwamba Marekani ni dola la kibeberu.  Na watawala wa mataifa ya Kiarabu wamezidi. Wamebobea kwa kujipendekeza kwa Marekani na kwa kuwa tayari kutumiliwa na dola hilo dhidi ya maslahi yao.

Alipokuwa akifanya kampeni yake ya uchaguzi wa urais mwaka 2016 Trump alikuwa akisema kinaganaga kwamba msimamo wake ni wa kutoiingiza Marekani vitani, kokote kule.

Trump anashikilia kwamba hataki vita na Iran.  Tunavyosikia ni kwamba Jumatano iliyopita alimwambia kwa ukali kaimu wa waziri wake wa ulinzi, Patrick Shanahan, kwamba hataki kuukuza ugomvi na Iran.

Aliyasema hayo katika Ikulu ya White House alipokuwa akizungumza na washauri wake wakuu juu ya majeshi ya Marekani yaliyo Mashariki ya Kati. Inasemekana kwamba ni yeye Trump aliyeanza kuidhukuru Iran.

Juu ya hayo, Trump ni Trump. Akili zake zinamtosha mwenyewe. Kwa sasa anaota, tena anaota ndoto za mchana akifirikia kwamba kwa kuitia ndaro Iran, watawala wa Teheran watasalimu amri na kumridhia kwa ayatakayo.

Wairan wanasema: “Yaguju!” Wameongeza kusema kwamba wao pia hawataki vita lakini wakishambuliwa watalipiza kisasi.

Wanasema kwamba kuwako kwa manowari ya Marekani na mbwembwe zake zote karibu na Iran ni usanii tu wa “kukikuza kivuli cha vita”.

Kamanda wa kikosi cha anga cha Jeshi la Mgambo la Kiislamu Brigadia-Jenerali Amir Ali Hajizade alisema hivi majuzi kwamba “zamani tukitishika kwa kuwako kwa manowari ya kivita ya Marekani karibu nasi ikibeba wanajeshi 6,000 na ndege za kivita 50 hadi 60. Leo si kitisho tena, ni shabaha.’

Trump hapendi kusikia maneno kama hayo.

Jumapili iliyopita aliandika kwenye akaunti yake ya twitter kwamba Iran ikiendelea kuitishia Marekani itakiona cha mtema kuni. Hapatokuwa tena nchi iitwayo Iran. Wakati huohuo anasema kwamba hataki vita na Iran.

Inaweza ikawa kweli hataki kupigana na Iran lakini anaweza akaingizwa mtegoni na watu kama Bolton na waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo. Wote hao wanawashwa pawepo vita, Iran ishambuliwe.

Na tusivisahau vitimbakwiri vingine. Kwanza kuna Israel nchi yenye kuichukia bila ya kiasi Iran na yenye ushawishi mkubwa kwa Trump. Nyuma yake kuna nchi vishawishi kama Saudi Arabia na Muungano wa Tawala za Kifalme za Kiarabu (UAE).

Kina Bolton wanatafuta kisingizio, kijisababu  cha kumchochea Trump apige firimbi ya kuanzisha vita dhidi ya Iran.

Usiku wa Jumapili iliyopita kombora la roketi liliripuka karibu na ubalozi wa Marekani, jijini Baghdad, Iraq. Ubalozi huo uko katika lile eneo liitwalo “Ukanda wa Kijani” (Green Zone). Hilo ni eneo lenye ulinzi mkali. Niliushuhudia kwa macho yangu jinsi ulivyo mkali mwishoni mwa 2017 kwani hoteli niliyoshukia Baghdad, Rashid Hotel, imo ndani ya ukanda huo na karibu kabisa na ubalozi wa Marekani. Jee, shambulio hilo lilikusudiwa wasingiziwe marafiki wa Iran walio Baghdad ili iwe kijisababu cha kuikhambulia Iran?

Mwishoni mwa wiki iliyopita Israel ilirusha makombora kadhaa kuupiga mji mkuu wa Syria, Damascus. Jee, ikitaraji kwamba Iran itaisaidia Syria kwa kulipiza kisasi dhidi ya Israel na hivyo kuipa Marekani kisingizio cha kuishambulia?

Kabla ya hapo, meli moja ya Saudia ya kubebea shehena za mafuta ilitobolewa katika bandari moja katika nchi za Ghuba.  Saudi Arabia ikaruka na kusema Iran lazima ishikishwe adabu kwa tukio hilo.

Iran itaendelea kusingiziwa kwa hili na lile ili papatikane kijisababu cha Marekani kuishambulia.

Marekani haiwezi kupeleka wanajeshi wake Iran lakini itatumia ndege za kivita zilizo kwenye manowari yake katika Ghuba kuitwanga Iran kwa mabomu na makombora.

Lugha inayotumiwa siku hizi na watawala wa Marekani na wa Saudi Arabia ni ya kuashiria kwamba Iran imekosa na inastahiki kutiwa adabu. Nchi hizo mbili zinasema kwamba hazitaki vita na Iran lakini zinajiandaa kupambana na kitisho cha Iran. Hazisemi kitisho hicho ni kipi.

Kina Bolton, wakichochewa na Saudi Arabia na Israel, ndio waliochongea Marekani ikapeleka manowari yake katika Bahari ya Sham.

Marekani ikiishambulia Iran eneo zima la Mashariki ya Kati litaripuka.

Jambo ambalo kina Bolton hawalitambui ni kwamba ikishambuliwa, Iran inaweza ikaiumiza vibaya sana Marekani na huenda shambulizi hilo likasababisha kuporomoka kwa tawala za Saudia, Falme za Kiarabu na Bahrain, ambazo ni washirika wakuu wa Marekani.

Pingine Iran haina uwezo wa kufika Marekani na kulipiga mabomu dola hilo kubwa duniani. Lakini tangu Iraq ivamiwe 2003 Iran imekuwa ikijiandaa kwa siku itaposhambuliwa na Marekani.

Kuna hatua kadhaa inazoweza Iran kuchukua na athari zake zitakuwa kama zilzala itayoutikisa uchumi wa dunia nzima.

Hatua ya mwanzo inayoweza kuchukua ni kuuziba mlango bahari wa Hormuz ili kuzuia meli zibebazo shehena za mafuta zisiweze kupita.

Hatua nyingine huenda ikawa ni kuvilenga visima au mabomba ya mafuta au ya gesi ya nchi rafiki wa Marekani katika Mashariki ya Kati.

Endapo Iran itazichukua hatua hizo tutaraji kwamba hata nchi zetu ambazo ugomvi huo wa Marekani na Iran hauzihusu ndewe wala sikio nazo pia zitaathirika vibaya. Maisha yatazidi kuwa makali kwa kupanda kwa bei za mafuta yatayoadimika.

Wataibuka wananchi sehemu mbalimbali za Arabuni wataozisaili serikali zao kwanini zinatumiwa na Marekani na Israel.

Mchafukoge utaozuka hausemeki.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwenye gazeti la Raia Mwema la Mei 22 – 28, 2019.

 

 

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.