Kuna baya zaidi katika Muungano kuliko hizo kero

Moja ya taarifa za hivi karibuni kabisa kuhusu utatuzi wa kero za Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulioundwa Aprili 1964 ni ile inayohusu Zanzibar sasa kushiriki masuala ya kimafaifa.

Ya pili ni kutoka kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mussa Simai, aliyoitoa Bungeni tarehe 16 Aprili mwaka huu wakati akijibu swali la Mbunge Abbas Ali Hassan kutoka Zanzibar juu ya kero zipi za Muungano zimepatiwa ufumbuzi katika awamu hii.

Jawabu lilikuwa ni kero mbili: moja ni utafutaji na uchimbaj mafuta na gesi na pili ni kodi ya Ongezeko la Thamani ya (VAT) kwa asilimia sifuri kwa umeme unaouzwa na Shirika la Umeme la Tanzania Bara (TANESCO) kwa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO).

Juhudi mfano wa hizo katika kuhakikisha Muungano wa miongo mitano na nusu unakuwa wa usawa kwa pande zote zimeshawahi kufanywa, lakini bahati mbaya ni kuwa hazijawahi kufanikiwa kuzima malalamiko ya Wazanzibari juu ya Muungano wenyewe. Matokeo yake, kumekuwa na harakati nyingi kutoka Zanzibar kuhakikisha mabadiliko makubwa yanapatikana.

Nitakupa mifano miwili kama sehemu ya harakati hizo: tarehe 25 Oktoba 2018, Kamati ya Hoja ya Kura ya Maoni ya Zanzibar iliandika barua ikiitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuitisha kura ya maoni kuhusu Muungano. Sehemu ya barua hiyo inasema: “Katika taarifa tumeeleza kwa ufupi jinsi Zanzibar ilivyokuwa ndani ya siku 137 baada ya kupata Uhuru kutoka kwa Waingereza tarehe 10 Disemba 1963. Zanzibar ilipotea tena ilipotumbukizwa ndani ya Muungano na Tanganyika bila ya mashauriano yoyote na watu wa Zanzibar na Wawakilishi wao”.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa kamati hiyo, nakala ya barua ilipelekwa pia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Mkuu wa Mabalozi nchini Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa SMZ.

Pia taarifa juu ya uwepo wa barua hiyo zimefikishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Pili ni kuwepo kwa kesi katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) iliyofunguliwa na Wazanzibari elfu 40.Wakihoji juu ya uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kesi bado ipo.

Haya yote yanaashiria uwepo wa harakati kubwa za Zanzibar kuhakikisha ile wanayoamini ni haki yao kuhusu Muungano inapatikana ikiwa ni kwa mahakama au kura ya maoni.

Hapo sijawazungumzia Masheikh wa Uamsho walivyoendesha harakati za kutaka mabadiliko juu ya Muungano, hadi utawala ukaamua kuwanyamazisha na kila mmoja anaona walivyonyamazishwa.

Kwa nyakati tofauti, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar zimekuwa katika jitihada za kuutoharisha Muungano. Swali la kujiuliza: kwa nini bado malalamiko hayapungui na badala yake ndio kwanza yanaongezeka kila uchao hasa kutoka raia wa Zanzibar?

Nataka niwe mkweli hapa: ni matarajio ya ajabu mno, tena yasiyo na macho, kufikiria kwamba Wazanzibari watanyamaza kuulalamikia Muungano siku tu zikifutwa kero zote. Kama hujanielewa, twende wote. Tutaelewana tu!

Kuna wanasiasa na wasomi wakubwa hudhani kufutwa kwa kero ndio suluhisho la kila kitu, lakini kuamini huko ni kujidanganya. Tatizo kubwa na baya kuhusu huu Muungano ni hali mbaya za kiuchumi (umasikini uliokithiri) hata baada ya nusu karne ya uwepo wake.

Hali mbaya za kimaisha kwa raia hufanya wajiulize Muungano una faida gani? Ukichunguza wengi  wao hawahoji tena kuhusu kero, ila wanahoji uhalali wake, kura ya maoni na uhuru wa Zanzibar.

Na binaadamu akiwa haoni faida ya jambo fulani, hata ulipambepambe, bado hutobadilisha maamuzi ya moyo wake.

Ubovu wa maisha unaotokana na mikakati mibovu ya watawala ndio jambo baya mno kuliko hata hizo kero. Watu wameishi katika umasikini kwa miaka mingi, wakiwa ndani ya chombo kiitwacho Muungano.

Waafrika wengi wana njaa, umasikini na ufukara. Kelele za maandamano ya raia hutokana na kuchoshwa na ugumu wa maisha unaotokana na kushindwa kwa viongozi  kuyabadilisha maisha yao.

Tengeneza picha ya Zanzibar iliyoneemeka, wananchi wanayafurahia maisha yao, mtu hula atakacho kwa wakati atakao, umasikini unatokomea, watoto wanasoma vizuri na huduma za kijamii zipo muda wote.

Hayo yote yakawa yametokana na uongozi bora wa pande zote huku rais wa Muungano akiwa ndiye kaka mkubwa wa mambo yote.

Naamini malalamiko kuhusu Muungano yasingekuwepo, na hata kama yangezushwa, basi sio kwa hoja hizi za sasa kutoka Zanzibar, kwamba Zanzibar inanyonywa.

Lakini ikiwa bado Wazanzibari wanaishi katika umasikini uliokithiri, katu tusifikirie waatacha kuulalamikia Muungano, hata kero zote ziondoshwe. Huo ndio ukweli!

Kuna wakati utawala unakosa sifa kulaumu raia wake pindi wakianzisha harakati fulani. Hizi harakati hazianzi kwa bahati mbaya. Ni matokeo ya kukosekana utawala bora wa kuwanufaisha wananchi wake kwa kuwakwamua katika tope la umasikini uliofurutu ada.

Sina maana kero zisiondoshwe. La hasha. Ila wale wanaofikiria kuziondosha ndio suluhisho, waache fikra hizo. Ili malalamiko juu ya Muungano yapunguwe kutoka Zanzibar, kufuta hizi kero kuende sambamba na maendeleo ya wananchi. Pengine itasaidia!

Tena sio maendeleo ya nambari na kwenye karatasi, ila yaonekane na wananchi wajione kweli umasikini umepungua. Vyenginevyo tutarajie harakati na miamko mingi zaidi ya kuhoji uhalali wa Muungano, kesi mahakamani na kudai kura ya maoni.

TANBIHI: Makala hii ya Rashid Abdallah ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 2  Mei 2019.

 

 

 

Author: Weyani Media

Weyani Media Production (WMP) is a media company which deals with organisation of news stories, exclusive interviews, media events, documentaries, image presentation, photo shooting, video production, special coverages and media media consultancy.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.