Sikukuu ya Kizanzibari na Hina: Picha Moja, Maneno Alfu Moja

Nililazimika kujipa muda wa takribani dakika kumi kuitafakari picha inayotembea mitandaoni ikiwaonesha watoto wanaopakwa hina kama kiashirio cha jambo kubwa na la kipekee mbele yao, lakini baada ya kujipa muda huo nikaanza kujilaumu kwa kuusaliti moyo wangu kwa uamuzi usio wa busara na ambao huenda nisipate tena fursa ya kuurekebisha kwa miaka ya karibuni!

Awali nilishapanga kuzuru kisiwani Pemba mwanzoni mwa wiki hii. Ilikuwa nishaunong’oneza moyo wangu kuwa hiyo ingekuwa mojawapo ya safari nitakazozifurahia maana ningekwenda kujenga mnara mpya wa kumbukumbu nitakaoweza kuja kuusimulia baadaye.

Kuna mambo mawili yaliyotaka kunisukuma kuzuru Kisiwani humo katika kipindi hichi cha kuelekea Sikukuu ya Eid-ul-el Fitr, wenyewe twaiita Skukuu ya Mfunguo Mosi: Moja ni kiu ya kuwaona wazee wangu na pili ni hamu kula sikukuu Kisiwani humo hasa kwa kufuata zile hisia za kila mtu anayeishi Pemba, kujiona anawajibikiwa na sikukuu yenyewe. Na chambilecho ami yangu, Rashidi Dume: “Skukuu hasa i Pemba. Unguja kuna watu na magari yao tu!”

Picha kwa hisani ya ukurasa wa Facebook kwa Mwarabu Seseme Ramadhan.

Naam, ukiyatazama mazingira yaliyopo ndani ya picha niliyoitaja (na iliyopamba makala hii hapo juu), ni rahisi kukubaliana na maneno ya ami yangu hata kama picha yenyewe haijioneshi kuwa imepigwa katika upande upi wa visiwa hivi, ukizingatia kuwa Unguja na Pemba ni watoto wa mama mmoja.

Kwa historia ya tokea enzi za mababu na mabibi zetu, sikukuu ni tukio linalobeba hisia za rika zote. Huyu atashika n’chi, yule kitambaa na chungio, huyu kipande cha limau na wewe ukiwa na kopo la maji ukikosha kinu, ilimradi tu mama, dada, bibi au ndugu yako wa kike aipate hina itayomchoresha msumeno au mtindo mashuhuri wa bararabara mguuni.

Usisikie la kuambiwa, hali hii ilileta ladha hata kwa wewe mwanamme wa miaka 40, maana sikukuu ni siku inayowakilisha hisia kuu za kiimani na kimwili kwa yule inayemuwajibikia na wawajibikao kwetu Pemba huwa wengi. Binafsi, sitosahau matukio kadhaa ya zama hizo za umri wa utotoni mwangu ambapo nikiongozana na wenzangu, wake kwa waume, tulivyokuwa tukitamba majiani na mifuko ya Rambo kuusaka muhina ulipo, kuchuma majani yake kwa ajili ya dada zetu na vipenzi vyetu, mfano wa watoto wa wajomba na maami. Unajiuliza ujira ni upi? Ujira ni dada au mtoto wa shangazi afurahi sikukuu. Na huo ndio upekee wake. Furaha ni yake, ridhiko ni lako.

Jicho ndani ya Insha ya Picha

Naam, turudi kwenye picha yenyewe kama ilivyosambazwa machoni mwetu kupitia mitandao ya kijamii. Mithili ya mwalimu anayegawa karatasi za mitihani kwa wanafunzi wake, ndivyo tunapobaini kuwa huu ni mtihani wa Kiswahili unaomtaka kila mwanafunzi aandike insha ya picha.

Picha kwa hisani ya ukurasa wa Facebook kwa Mwarabu Seseme Ramadhan.

Tukopezane tu kidogo kuwa kwenye insha ya picha, mwanafunzi hupewa michoro au picha na kutakiwa atunge insha yake kulingana na muonekano wa picha hiyo. Tukopezane tena kabla ya msimamizi hajaingia darasani, ni kwamba utungaji huo unayataka mawazo yetu yafungamane na tafsiri ya michoro au picha tuliyopewa.

Hata hivyo, kumradhi ikiwa hapa hutaona simulizi yangu ikiielezea picha husika na vile vilivyo ndani yake kwa utamaduni na mila za kwetu mbele ya kitu hina. Lakini utakubaliana nami kwamba kusambazwa kwa picha yenyewe kumekuja katika kipindi ambacho tulipaswa kujitafakari kama tufanyayo ni mema na yana tija kwa mustakbali wa vizazi vyetu.

“Mkaidi Hafaidi ila Siku ya Idi”

Kutokana na mvuto wake, wengi tumejikuta tukiwa mawakala wa kuisambaza picha ya watoto waliopangwa foleni wakipakwa hina. Wengine wamefikia mbali kwa kuiandikia na ujumbe mfano wa Zanzibar Culture – utamaduni wa Zanzibar!

Picha kwa hisani ya ukurasa wa Facebook kwa Mwarabu Seseme Ramadhan.

Lakini swali la kujiuliza na kutusuta ni je, utamaduni huo bado upo? Binafsi, siamini kuwa ungalipo. Ni sawa na mambo yetu mengi yaliyokufa na ambayo awali yalilenga katika kuutambulishia upekee wa taifa letu la Zanzibar. Kutoka hina ya kutwangwa kwa kinu, wanja ya kombe, futari ya pamoja mitaani, kuamshana daku kwa pembe, baraza za nyumba zilizokuwa ukumbi wa wazi wa mikutano, vikao, na pia darasa, na mengi mengineyo, picha hii ya hina inatukumbusha kuwa Zanzibar imepoteza mengi yaliyoifanya iwe Zanzibar.

Pengine tumepoteza kwa ukaidi wetu, au pengine kwa ugoigoi wetu – wa kudhani kwamba kila kisemacho kuhusu sisi ni cha kishamba na kila kijacho kutoka ugenini ndicho cha kimjini. Lakini ukweli ni kuwa picha hii ina ujumbe mkubwa: “Mkaidi Hafaidi Ila Siku ya Idi”. Na kwa hivyo, kama ulikuwa ni ukaidi wetu, Idi ya mara hii imetufaidisha kwa kutuambia kuwa, kwa pamoja, tunapaswa kutafakari namna nzuri ya kulinda mila na tamaduni zetu kwa maslahi ya vizazi vyetu vya baadaye.

Hawakukosea Waswahili waliposema: “Kibaya chako tunza, cha mwenzako si chako.” Tukikaa na kupima athari inayopatikana ni kubwa na mbaya kufuatia jamii yetu sasa kutokuwa na mwamko wa kuzitunza mila, silka na utamaduni unaotutambulisha.

Eti leo tumekuwa sisi ndio wa kununua hina kutoka mataifa ya mbali, wakati tungeifufuwa mihina yetu na mengine kuipanda kwa wingi, huenda leo na kesho tukapata soko kubwa la hina katika mataifa ya Kiarabu, Amerika ya Kusini na Ulaya, ambako tungeutambulisha utamaduni wa hina ya Kizanzibari iliyo tafauti sana na hina ya kwengineko.

Bali hatujachelewa. Lau nia ipo.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Abdulwahab Mohammed Suleiman.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.