SUDAN: mpasuko jeshini ndio utaoyavua mapinduzi

MAMBO yamebadilika ghafla Sudan. Kwanza Wasudani wakitokwa na machozi ya furaha baada ya kuangushwa Rais Omar al Bashir Aprili 11.

Siku hiyo ulimwengu uliyashuhudia mapenzi makubwa baina ya wanajeshi wa ngazi za chini na wananchi waliokuwa wakiandamana dhidi ya utawala wa kijeshi. Ilionekana kama wananchi na wanajeshi walikuwa kitu kimoja kwenye safari moja ya kuelekea kwenye demokrasia.

Sasa mapenzi hayo yametoweka na machozi ya furaha yamekauka.

Tangu Jumatatu ya wiki iliyopita miji ya Khartoum na Omdurman imegeuka kuwa viwanja vya mauaji.  Baada ya kuwatawanya waandamanaji, kikosi maalum cha idara ya usalama kimekuwa kikiwaua.

Maiti wameonekana wakielea katika mto Nile walikotupwa na wanajeshi. Labda wamefanya hivyo ili idadi halisi ya watu waliowaua isijulikane.

Watawala wa kijeshi wakachukua hatua zaidi za kuwatia adabu wanamageuzi. Waliifunga intaneti, wakawatia mbaroni viongozi wa upinzani.

Wanaharakati wa kike wamelalamika kwamba wanajeshi wanawatisha kwamba watawabaka wasipoziacha harakati zao.

Wapinzani nao wakakataa kurejea kwenye mazungumzo na watawala.  Badala yake wakatangaza mgomo kuanzia Jumapili iliyopita na walisema hawatozitii amri za serikali mpaka itapoundwa serikali ya kiraia.

Siku ya mwanzo ya mgomo jiji la Khartoum lilikuwa kama lililokufa ganzi. Zahma za kawaida barabarani ziliyayuka.

Mabasi ya usafiri wa umma na teksi zote ziligoma. Hakuna kilichofunguliwa; si maduka, si ofisi, si kampuni za watu binafsi na si mabenki. Benki chache zilizofunguliwa zilikuwa za serikali.

Yote hayo hayashangazi kwani si mageni nchini humo.

Sudan ni taifa lisilotulia kwa muda mrefu. Limekuwa hamkani tangu lipate uhuru Januari 1, 1956.  Misuguano ya roho haishi baina ya kabila na kabila, baina ya makabila na serikali, baina ya majeshi na raia, baina ya serikali kuu na majimbo.

Kwa muda mrefu majeshi yamekuwa yakishika mpini wa utawala na takribani wakati wote yameushika kwa mikono ya chuma. Mara baada ya mara, yamekuwa yakipindua serikali na baada ya muda huwarejeshea raia panapokuwa shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi. Na wanapopata mwanya tu hujipenyeza na kuipindua tena..

Wakati mwingine wanajeshi hupinduana wenyewe kwa wenyewe kama ilivyotokea alipopinduliwa al Bashir, aliyetawala kwa karibu miaka 30 baada ya kuipindua serikali ya kiraia ya waziri mkuu Sadiq al Mahdi, kiongozi wa chama cha Umma.

Wanajeshi walimpindua al Bashir walipoviona vishindo vya umma uliopiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi ukimshinikiza ajiuzulu.

Masaibu mingine yaliyoikumba Sudan ni vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya makabila na baina ya serikali na wapiganaji wenye kutaka maeneo yao yapewe mamlaka zaidi ya kujiendesha.  Mapigano ya miaka nenda miaka rudi, kwa mfano, baina ya serikali na wapiganaji wa Sudan Kusini yalisababisha kumeguka kwa taifa hilo ilipozaliwa nchi huru ya Sudan Kusini Julai 9, 2011.

Asilimia zaidi ya 98 ya wakaazi wa Sudan Kusini walipiga kura ya maoni Januari 2011 wakiunga mkono eneo lao liwe nchi huru.

Hiyo iliyosalia kuwa Sudan iko ukingoni na huenda karibu ikatumbukia katika duru nyingine ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hofu ya kuzuka mapigano ya aina hiyo ndiyo iliyoushajiisha Muungano wa Afrika (AU) uichukulie hatua Sudan. Alhamisi iliyopita AU iliisimamisha Sudan isishiriki katika shughuli za Muungano huo mpaka itapounda serikali ya kiraia.

Kwa sasa Sudan inatawaliwa na Baraza la Kijeshi la Mpito linaloongozwa na Luteni-Jenerali Abdulfattah al Burhan, mwenye umri wa miaka 59. Aliushika uongozi wa utawala Aprili 12 baada ya kujiuzulu Luteni-Jenerali Ahmed Awad Ibn Auf aliyekuwa kiongozi kwa siku moja tu.

Wanamageuzi waliokuwa wamemiminika barabarani Khartoum na kwenye miji mingine ya nchi hiyo hawakumtaka kabisa Ibn Auf. Walisema alikuwa karibu sana na al Bashir. Kwa hivyo, walifurahi pale wenzake walipomuondosha wakamweka al Burhan badala yake.

Al Burhan aliyekuwa inspekta mkuu wa majeshi anaonekana kuwa ni mwanajeshi mwenye mikono safi isiyo na damu. Hatua ya mwanzo aliyoichukua aliposhika uongozi ilikuwa kuwafungua wafungwa wote wa kisiasa waliofungwa na al Bashir.

Kwa kufanya hivyo, al Burhan aliwafurahisha wanamageuzi na alizidi kuwafurahisha aliposisitiza kwamba analiunga mkono dai lao la kutaka utawala wa kiraia urejeshwe.

Lakini anayeonekana kuwa na nguvu zaidi ndani ya Baraza la Kijeshi ni naibu wake al Burhan, Jenerali Mohamed Hamdan Dagolo (maarufu kwa jina la “Hemedti”).  Hamna shaka yoyote kwamba Hemedti anaogopwa na Wasudani wenzake.

Hemedti aliibuka baada ya kuanza vita vya Darfur mwezi wa pili wa 2003. Makundi mawili ya waasi (SLM na JEM) yalikuwa yakipigana na majeshi ya serikali.  Waasi hao walikuwa wakiishtumu serikali kuwa ikiwabagua Wasudani wasio na asili ya Kiarabu.

Hemedti ni mwenyeji wa Darfur na ana asili ya Kiarabu. Ukoo wake ni wa Awlad Mansour (watoto wa Mansour) wa kabila la Mahariya.

Wakati wa vita vya Darfur Hemedti aliyaongoza majeshi ya mgambo ya Janjawid yaliyokuwa yakitumiwa na serikali kupigana na waasi. Serikali ilimuajiri Hemedti na watu wake mwaka 2003 na iliwapa silaha ili wapigane na wahakikishe usalama wa mji wa Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

Kabla ya hapo, Hemedti, anayesemekana kuwa hakuhitimu masomo ya skuli ya msingi, alikuwa akiuza ngamia jangwani kama baba yake.

Safari moja, mmoja wa misafara yake ulishambuliwa na watu wa kabila la Zaghawa, kabila la Kiafrika ambalo pia ni kabila la Rais Idriss Deby wa Chad.  Wazaghawa hao walimuibia Hemedti mifugo (ngamia na ng’ombe) 3,400, na waliwateka nyara watu 77, wakiwa pamoja na jamaa zake 10.

Hemedti akawa na kisasi cha kulipiza.  Ndipo serikali ilipoamua kumtumia aisaidie kupambana na waasi. Hemedti hakukataa. Aliwakusanyakusanya watu wa kabila lake na akawaingiza katika jeshi la mgambo lililoitwa Janjawid.

Wengi wa wanamgambo hao walikuwa ni Waafrika wenye kujihusisha na Uarabu pamoja na idadi ndogo ya Mabedui wa kabila la Kiarabu la Rizigat. Lakini makabila mengi ya Kiarabu hayakujihusisha na Janjawid.

Wanamgambo wa Janjawid wameshtumiwa kuwaua maelfu kwa maelfu ya watu katika eneo hilo la magharibi mwa Sudan.

Wameshtumiwa pia kwa ubakaji wa wanawake, udhalilishaji wa watu kwa ubaguzi wa kikabila, kuviziba visima vya maji na wizi wa mifugo pamoja na mali nyingine za wakaazi wa Darfur.

Hemedti anatuhumiwa kuwa ndiye aliyekuwa akivisimamia vitendo hivyo lakini anakanusha. Anasema kwamba alikataa kufuata amri za kushambulia sehemu wanazoishi raia .

Anachokiri ni kwamba aliombwa na al Bashir binafsi aongoze mashambulizi dhidi ya waasi.

Vitendo vya kinyama vya wanamgambo hao ndivyo vilivyomsababisha al Bashir ashtakiwe na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) kwa makosa ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita, pamoja na makosa ya jinai dhidi ya ubinadamu

Serikali ya al Bashir daima ilikuwa ikikanusha kwamba ikihusika na Janjawid. Hata hivyo, inasemekana kwamba upo ushahidi wenye kuthibitisha kwamba al Bashir aliwateua mawaziri wake wawili na wakuu wengine wa serikali wawe waratibu baina ya majeshi rasmi na wanamgambo hao.

Mwaka wa 2013 Janjawid waliingizwa rasmi kwenye kikosi maalum cha idara ya usalama ambacho ndicho chenye kuwakandamiza waandamanaji.

Ingawa alikuwa karibu sana na al Bashir, Hemedti alimgeukia katika siku zake za mwisho madarakani.  Amekuwa akisema kwamba naye pia anawaunga mkono wanamageuzi.

Hata hivyo, wachunguzi wengi hawayaamini ayasemayo na wanamtilia shaka yeye na al Burhan kwamba wana ajenda yao ya siri dhidi ya wanamageuzi.

Ukandamizi wa kikosi cha usalama uliendelea hata alipokuwako Khartoum waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, aliyekwenda huko akiwa mjumbe wa AU kutafuta suluhu baina ya Baraza la Kijeshi na wanamageuzi.  AU pamoja na kuisimamisha Sudan isishiriki katika shughuli zake pia imewatishia kuwawekea vikwazo viongozi binafsi wa Sudan wataobainika kuwa ndio wenye dhamana ya sokomoko liliopo nchini humo.

Ingekuwa vizuri lau AU ingeweza kupeleka jeshi la kuweka amani lakini Muungano huo hauna uwezo huo kwa sasa.  Na jeshi la Sudan lina nguvu.  Inaelekea pia kwamba watawala wa kijeshi watavipuuza vitisho vya AU kwani wanazitegemea sana nchi za Saudi Arabia na Tawala za Kifalme za Kiarabu (UAE) kwa misaada.

Kwa hakika, dhana iliyopo ni kwamba nchi hizo mbili za Ghuba pamoja na Misri ndizo zinazowashikilia watawala wa kijeshi wa Sudan wazidi kukaza kamba wanapokutana na wanamageuzi. Nchi hizo zinaogopa kwamba nguvu za umma wa Sudan zikishinda zisije zikawaambukiza wananchi wao.

Hali iliyopo Sudan ni ngumu kwa wanamageuzi. Ni mpasuko tu ndani ya jeshi utaoweza kuyafanikisha mapinduzi yao endapo patazuka wanajeshi wataowaunga mkono moja kwa moja dhidi ya kina Hemedti.

TANBIHI: Makala hii imeandikwa na Ahmed Rajab na kuchapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 12-18 Juni 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe:aamahmedrajab@icloud.com; Twitter:@ahmedrajab

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.