“Nisamehe, Bwana Rais”

MAMBO mengi ya kijinga huzuka serikali inapokuwa haina akili.  Inapojifanya hamnazo ikiwa inajaribu kuuzuga ulimwengu kwa ujinga inaoufanya. Siku hizi tunayashuhudia hayo yakichomoza kwingi duniani. Na huchomoza takriban kila siku.

Yanatokea katika nchi zenye mifumo tofauti ya kiutawala, katika nchi za kaskazini na za kusini, za magharibi na za mashariki.

Na Ahmed Rajab

Mfano mmoja wa ujinga ninaouzungumzia ni ule wa Rais Donald Trump wa Marekani. Amesema mengi ya kijinga na amechukua hatua kadhaa za kijinga na zenye kuhatarisha usalama wa dunia.  Ujinga wake ni pamoja na hatua yake ya kujitoa kutoka mapatano yaliyofikiwa na Iran kuhusu suala la nyuklia. 

Tunasikia kwamba alifanya hivyo kwa sababu ya chuki zake binafsi dhidi ya rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, aliyesaidia kufanikisha mapatano hayo.

Na la Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamaganda Kabudi, nalo si mdogo.  Vipi unasema jambo dunia nzima likalisikia na halafu ukalikana kama hukulisema?  Dunia iliyadaka matamshi yaliyomdondoka alipohojiwa na kipindi cha Focus on Africa cha BBC na akisikika akisema kwamba mwanahabari Azory Gwanda amefariki.

Baadaye Kabudi alikuja kwa matao ya chini akisema kwamba hakusema aliyoyasema ila alinukuliwa vibaya.  Gwanda hajulikani alipo tangu Novemba 21, 2017.  Amepotea kama moshi hewani. 

Uzito wanaoufanya watawala ni kutoonekana kuwa na juhudi za kufuatilia kadhia Gwanda na ya wengine waliopotea nchini Tanzania.  Hii ni kashfa kubwa kwa Tanzania.

Uzito mwingine wa watawala ni wa kuwatumia watu dunia nzima ikiwa inajua kuwa watu hao wanatumiliwa kuwakorofesha na kuwakashifu wakosoaji wa serikali au wenye kudhaniwa tu kuwa ni wapinzani.

Miongoni mwa waliochafuliwa ni waziri wa zamani ya mambo ya nje Bernard Membe na makatibu wakuu wastaafu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana.  

Tuliianza wiki kwa kuusoma waraka mzito ulioandikwa na kusainiwa na Makamba na Kinana ukimtuhumu  mtu aitwaye Cyprian Musiba kwa kuwachafulia majina yao.

Waraka huo ni dalili ya kimbunga kinachokuja ndani ya CCM.  Tufani hiyo ikivuma basi itakuwa imesababishwa na ujinga wa baadhi ya viongozi wa CCM yenyewe.

Kwa ufupi, ujinga umetanda kama wingu lenye kuzigubika tawala mbalimbali. Hata hivyo, ujinga huo unashtadi na kuwa na hatari zaidi katika nchi zenye serikali zilizo na muelekeo wa kimabavu, ama kwa kuwa mfumo wao wa kiutawala ni wa kimabavu au kwa kuwa viongozi wao wakuu ni wenye kutenda mambo kibabe ubabe.

Ujinga aina hiyo ndio unaowafanya wale wenye kuishi katika tawala zilizo chini ya madikteta wawe wanawatamani viongozi waliotangulia hata kama hao pia walikuwa na dosari zao.  Baadhi yao walikuwa wakitawala kimabavu pia. Mfano mzuri ni wa Hosni Mubarak aliyekuwa rais wa Misri kwa miaka 30 tangu 1981 hadi alipopinduliwa na nguvu za umma 2011.

Rais Abdel Fattah al Sisi, anayetawala sasa amempiku Mubarak, kwa kutawala kimabavu na kwa kuendesha uchumi kwa namna inayoyafanya maisha ya mwananchi wa kawaida wa Misri yazidi kuwa makali.  Wananchi wanalalamika, wanapiga kelele lakini waafanya hivyo zaidi kwa kunong’ona kwa sababu wanauogopa utawala wa al Sisi usije ukawachukulia hatua kali.

Baada ya al Sisi na wanajeshi wenzake kumpindua Mohamed Morsi, aliyekuwa rais wa kwanza katika historia nzima ya Misri kuchaguliwa kidemokrasia, wananchi wengi wa taifa hilo wakimuona al Sisi kuwa kama mwokozi wao.

Wamisri walikuwa hawakujua kwamba Morsi alitegwa na kina al Sisi waliousambaratisha kwa kusudi utawala wake. 

Hivi sasa nchini Misri kuna wanaomtamani Morsi afufuke arudi madarakani na kuna wanaozitamani enzi za hata Mubarak.  Wote hao wanaonekana kuwa ni afadhali kuliko huyu wa sasa.

Ndipo wenye akili zao walipoamua kuanzisha ukurasa kwenye mtandao wa Facebook wenye anuwani ya  “Nisamehe, Bwana Rais”.  Ukurasa huo, ulioanzishwa Februari 2011, unamsifu tu Mubarak na unamtaka radhi kwa namna alivyokuwa akikosolewa na kupingwa alipokuwa madarakani.

Kwa kufanya hivyo unakuwa unamlinganisha na al Sisi na kwa kuwalinganisha viongozi hao wawili ujinga wa al Sisi na wa utawala wake unazidi kudhihirika.  Vipande vya video vya zamani vya Mubarak hupachikwa kwenye ukurasa huo ili kuwakumbusha Wamisri mambo yalivyokuwa chini ya Mubarak na yalivyozidi kuoza hivi sasa.

Wapambe wa al Sisi na vibaraka wake wameliona hilo na Alhamisi ya wiki iliyopita walimtia mbaroni msimamizi wa ukurasa huo wa Facebook, Karim Hussein. Mshitaki mkuu wa serikali aliamrisha Hussein awekwe kizuini kwa siku 15 ili kuendelea na uchunguzi kuhusu “kusambaza habari za uongo”. 

Huo nao ndio ujinga mwingine unaofanywa na utawala wa al Sisi.  Hauwezi kuvumilia usikoselewe hata kama ukosoaji mwingine hufanywa kwa stihizai au kwa mizaha.

Wiki iliyopita dunia iliyashuhudia mengi mengine ya kijinga. Nchini Sudan Baraza la Muda la Kijeshi linalotawala huko lilitangaza Alhamisi iliyopita kwamba liliufuma mpango wa kutaka kulipindua.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa wanajeshi kudai kwamba wameugundua mpango wa kuwapindua. Walishatoa tangazo kama hilo mara mbili mwezi uliopita. Walisema kwamba jaribio moja la kupindua lilifanywa na wafuasi wa al Bashir na jengine lilifanywa na wapinzani. Hakuna ushahidi walioutoa.

Bila ya ushahidi kutolewa ilikuwa dhahiri kwamba watawala wa kijeshi wakitaka kuuhadaa ulimwengu kijinga kwamba Baraza la Mpito la Kijeshi limo hatarini na linaweza wakati wowote likapinduliwa na wanajeshi wenye vichwa mchungu zaidi ya wajumbe wa Baraza la Mpito.

Kwa hivyo, hatukushangaa hivyo watawala wa kijeshi walipotangaza Alhamisi iliyopita kwamba wameigundua hiyo njama ya kutaka kuwapindua. Zaidi kilichotufanya tusishangae hivyo ni kwa sababu kama tulivyoashiria katika toleo lililopita la Raia Mwema tunajua kwamba kuna mgawanyiko ndani ya jeshi. 

Jeshi la Sudan lina mirengo na mapande tofauti yenye kukinzana. Miongoni mwayo ni lile lenye kumuunga mkono Rais aliyepinduliwa na jeshi lenyewe, Omar Hassan al Bashir. 

Pande hili lina nguvu kubwa ndani ya jeshi. Vilevile lina nguvu na ushawishi mkubwa ndani ya vyombo vingine vya usalama, hasa lile jeshi maalum la mgambo (RSF), lenye kuongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo (Hemeti), na kwenye Shirika la Ujasusi na Usalama (NISS).  Huo ni uwezo uliojipangia kwa muda wa zaidi ya miaka 30.

Hivi sasa pande hilo linajaribu kuutumia uwezo huo ili kuwaangusha waliomuangusha al Bashir.  Moja ya njia za kufikia lengo hilo ni kuandaa mipango ya chini kwa chini ya kuyachimba yale mapatano yaliyofikiwa karibuni baina ya Baraza la Mpito la Kijeshi na muungano wa wapinzani.

Baada ya kuyakubali hayo mapatano wanajeshi sasa wanajuta. Wamo mbioni wakijaribu kufanya kila njia ya kuyazuia yasitekelezwe.  Kwanza hadi hivi tunapoyaandika makala haya, hayo mapatano hayakutiwa saini na wanajeshi.

Saa kadhaa kabla ya wakati wa kutiwa saini mapatano hayo ndipo wanajeshi walipotangaza kwamba wameufuma mpango wa kutaka kuwapindua na waliwakamata wanajeshi 12. Hakuna maelezo ya kina yaliyotolewa kuhusu njama hiyo wala watawala wa kijeshi hawakutoa ushahidi wa kuthibitisha dai lao.

Kuna tetesi kwamba hilo tangazo la wanajeshi la kwamba walitaka kupinduliwa lilikuwa lenyewe ni njama ya wanajeshi kujipa muda ili waweze kujizatiti zaidi katika mazungumzo na wapinzani wa kiraia kuhusu namna ya kuhodhi pamoja madaraka.

Hata hivyo, tunasikia pia kwamba wanajeshi wenye kumuunga mkono al Bashir walikuwa kweli na azma ya kupindua. Waliizungumza na kuijadili azma hiyo lakini walikuwa hawakufika mbali na mipango yao.

Wafuasi wa al Bashir wanajaribu kuyazuia mapatano hayo yasitekelezeke kwa sababu endapo mapatano hayo yatasimama basi huenda yakawa pigo kubwa kwa maslahi yao.  Jeshi maalum la mgambo la RSF pamoja na mkuu wake Hemeti wana rasilmali nyingi walizowekeza katika migodi ya dhahabu.

Wanajeshi wanahofia pia kwamba taasisi zitazoanzishwa wakati wa kipindi cha mpito huenda zikawaathiri vibaya kwa vile zitaanza kuchukua hatua kuhusu mambo ya uwazi na uwajibikaji.

Hofu kubwa ya wanajeshi ni kupandishwa mahakamani kuyakabili mashtaka ya mauaji ya waandamanaji mnamo Juni 3 na pia kuhusu shutuma za ufisadi pamoja na wizi wa mali za umma.

Tunasikia kwamba wanajeshi walikipachika kifungu kimoja katika mapatano hayo ambacho kinatamka wazi ya kuwa wanajeshi wasishitakiwe wala wasipokonywe mali zao.  Watawala wa kijeshi wamekipachika kifungu hicho kwenye mapatano ili kiweze baadaye kuwalinda wasishitakiwe au wasiwajibike kwa vitendo vyao kabla na baada ya kuangushwa al Bashir.

Hatujui utawala wa kijeshi wa Sudan una lipi jingine la kutushangaza siku zijazo.  Kwa sasa umekaa kama hauna akili; unafanya mambo ya kijinga yenye kuhatarisha maisha ya watu.  

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 17 – 23 Julai, 2019. Mwandishi anapatikana kwa baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab

Author: Weyani Media

Weyani Media Production (WMP) is a media company which deals with organisation of news stories, exclusive interviews, media events, documentaries, image presentation, photo shooting, video production, special coverages and media media consultancy.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.