Rais wa Tanzania John Magufuli apokea dhahabu na fedha zilizokamatwa Kenya

Serikali ya Tanzania imepokea kilo 35.34 za madini ya dhahabu zenye thamani ya dola milioni moja za Marekani na fedha kiasi cha shilingi milioni 170 za Tanzania, dola za Marekani 76,500 na shilingi za Kenya 171,600, fedha zilizokamatwa nchini Kenya.

Mali hiyo ilikamatwa tangu mwaka 2004 baada ya kuibwa kwenye benki ya NBC tawi la Moshi.

Ujumbe wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ukiongozwa na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Monica Juma na Mkurugenzi wa mashtaka Nurdini Haji, umekabidhi madini na fedha hizo Ikulu ya Tanzania na kutoa ripoti kuhusu namna madini hayo yalivyokamatwa mwaka jana nchini Kenya.

Mkurugenzi wa mashtaka wa Tanzania, Biswalo Mganga, aliongoza timu ya watu 11 kuhakikisha dhahabu iliyokamatwa inarejea ili kuweza kutumika kama kidhibiti kwenye kesi inayoendelea kuhusu makosa ya uhujumu uchumi huko Mwanza.

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Monica Juma
Image captionWaziri wa mambo ya nje wa Kenya, Monica Juma

Dhahabu zilipatikanaje?

”Mnamo tarehe 15.2.2018 dhahabu ya kilo 35.34 wakati msafiri mmoja ajulikanaye kwa jina la Baraka Chaulo aliyesafiri na ndege ya shirika la Presicion akitokea jijini Mwanza, kisha kutua Kilimanjaro na baadae kuelekea Kenya alipokamatwa kwenye uwanja wa Jommo Kenyatta..taarifa zilipopatikana, mkurugenzi wa upelelezi wa Tanzania na mwenzake wa Kenya walishirikiana kufanyia upelelezi tukio hilo”.

Mganga amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Profesa Adelardus Kilangi aliandika maombi kwenda Kenya kuomba dhahabu hiyo irejeshwe.

Amesema pia taratibu za kumrejesha nchini kutoka Kenya mtu aliyeshiriki uvamizi katika benki ya NBC tawi la Moshi zilikwama kwa miaka mingi, lakini kwa ushirikiano kati yake na DPP wa Kenya, mshtakiwa huyo ameshejeshwa Tanzania na kesi yake iko Moshi.

Sheria kuhusu usafirishaji madini

Sheria za Usimamizi wa Forodha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) za mwaka 2004, kifungu 85(3) na Kiambatanisho cha Pili Sehemu B (4) huharamisha usafirishaji wa madini ambayo hayajapitia viwandani katika kanda ya Afrika Mashariki.

Naye Rais Magufuli baada ya kukabidhiwa dhahabu na fedha ameshukuru serikali ya Kenya kutekeleza jambo hilo.

Raisi John Magufuli
Image captionRaisi wa Tanzania John Magufuli

“Namshukuru Rais Kenyatta kwa upendo na uaminifu mkubwa alionao kwa kurejesha dhahabu yenye uzito wa kilo 35 pamoja na fedha, rais Uhuru amefanya kitendo cha kiungwana kwa kuturudishia madini yetu ambayo yalikuwa yametoroshwa.

“Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kazi kubwa walioifanya.”Tuliamua kuchukua hatua za makusudi za kuweka mikakati ya kulinda rasilimali zetu za madini ili ziweze kuwanufaisha Watanzania”.

Kwa mujibu wa rais Magufuli matukio ya utoroshaji wa madini nchini Tanzania yamefika 102 kwa mwaka uliopita pekee.

“Wa kupongezwa kwa hili ni vyombo vya Kenya, najua wakuu wa vyombo hivyo Tanzania mpo hapa, lazima niwatandike kwa sababu vitu vimetoka Mwanza vimekamatiwa Kenya. Je, vilipobebwa Mwanza na Kilimanjaro vyombo vyetu vilikuwa vinafanya nini?

‘Vitu vya fedha na dhahabu vinahitaji moyo wa jiwe, kiukweli Rais Kenyatta ni muaminifu, kwani vingeweza kupigwa, lakini fedha hizi zimerudi Tanzania baada ya miaka 15. Lakini na mimi mnipongeze, inawezekana wengine wangepiga dili juu kwa juu na wala msingejua.

Raisi John Magufuli azungumza na raisi Uhuru Kenyatta kwa simu

MAGUFULI UHURU

Ilikuwa hafla iliyosisimua kwani wakuu hawa wa nchi walizungumza kwa simu, baada ya Uhuru Kenyatta kumpigia Magufuli moja kwa moja wakati wa hafla hiyo.

Awali, Magufuli alimpigia simu Kenyatta lakini hakupokea, wakati akiendelea kuzungumza na viongozi mbalimbali waliokuwa wakishuhudia tukio la makabidhiano.

”Naona Kenyatta ananipigia,kumbe ameshapiga mara nyingi, maneno nayo ni matamu saa nyingine unasahau”. alisema Magufuli akiwavunja mbavu viongozi waliokuwa wakimsikiliza.

Rais Magufuli: Halooo

Rais Kenyatta: Mheshimiwa rais habari ndugu yangu?

Rais Magufuli: Nzuri bwana, mzigo umeshafika, mimi ninakushukuru sana.

Rais Kenyatta: Asante asante asante, tumesema kwamba mali ya wananchi wetu irudi kwa wananchi wetu.

Rais Magufuli: Sawa kabisa, endelea wanakusikiliza hapa.

Rais Kenyatta: Tumesema kwamba sisi kazi yetu ni kuhakikisha tumelinda mali za wananchi wetu na mali hiyo iweze kuwajengea wananchi hospitali, barabara, shule. Walaghai hawana nafasi kwa nchi zetu kabisa.

Rais Magufuli: Safi kabisa.

Rais Magufuli ameahidi kuwapatia zawadi wanausalama waliofanikisha juhudi za kukamtwa kwa wahalifu hao.

chanzo: bbc

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.